Meneja wa EWURA Kanda ya kaskazini, Injinia Lorivii Long’idu akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo hayo jijini Arusha
Meneja masoko wa kampuni ya Taifa gas, Joseph Nzumbi akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo hayo jijini Arusha leo.
………………………………………….
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Wafanyabiashara wanaouza gesi mkoani Arusha wametakiwa kutumia mizani kupimia wateja wao gesi ili waweze kupata ujazo ulioandikwa kwenye gesi husika.
Hayo yamesemwa Leo jijini Arusha na Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA)Kanda ya kaskazini,Injinia Lorivii Long’idu wakati akizungumza kwenye semina ya wasambazaji wadogo na wakubwa wa bidhaa za gesi jijini Arusha iliyoandaliwa na kampuni inayomiliki mitungi ya gesi ya Taifa na Mihan.
“Ni kosa kufanya biashara hiyo bila kuwa na mizani na kama hawana ni kosa la jinai na wakigundulika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao mara moja”amesema Long’idu.
Ameongeza kuwa, ni lazima wateja wauziwe gesi ambayo imepimwa na ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anajiridhisha kuchukua mtungi huo na kwenda kutumia ukiwa na ujazo unaotakiwa na uliopimwa kwenye mizani.
Ameongeza kuwa,wananchi wanatakiwa kutambua kuwa gesi ni salama kinachotakiwa ni kufuata taratibu na sheria zilizopo katika matumizi kwani gesi ni bora na salama .
“Nawaomba wafanyabiashara wahakikishe wanamuuzia mwananchi gesi kwa mujibu wa kilo iliyoonyeshwa kwenye gesi na lazima wapime kwenye mizani kiasi cha gesi, na ni kosa kufanya biashara bila kuwa na mizani.
Hata hivyo amewataka kuhakikisha wanatii sheria na kanuni za biashara hizo kwani matumizi ya gesi ni salama na yanasaidia kwa kiwango kikubwa kutunza mazingira .
“kuna wafanyabiashara ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wakipunguza mitungi mikubwa ya gesi na kupunguzia kwenye mitungi midogo na wanawauzia watu kiwango kidogo cha gesi tofauti na kinachotakiwa kwenye ujazo,tunaendelea na operesheni zetu na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.”amesema .
Ameongeza kuwa,hivi karibuni wamekamatwa wafanyabiashara wawili mkoani Kilimanjaro waliokuwa wanaenda kinyume na taraibu za EWURA kwa kupunguza gesi na kesi zao zipo mahakamani tayari na hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa.
Naye Meneja masoko wa kampuni ya Taifa gas , Joseph Nzumbi amesema kuwa,lengo la mafunzo hayo kwa wasambazaji hao wa gesi mbalimbali ni kupata uelewa wa kutosha jinsi ya kuendesha biashara hiyo huku wakifuata sheria na kanuni zilizopo ili kuweza kuondokana na majanga yoyote yanayoweza kutokea kupitia nishati hiyo.
Nzumbi amewataka wafanyabiashara hao kufuata misingi ya sheria na kanuni zilizopangwa na Mamlaka husika huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya nishati hiyo.