Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekitaka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuangalia uwezekano wa kupanua wigo wa Programu za Mafunzo inayotoa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kushika kasi duniani.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto pamoja na Watumishi wa Chuo hicho, katika siku ya tatu (3) ya ziara yake leo tarehe 18 Mei, 2022, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa dunia ya sasa mtu hapimwi kwa idadi ya vyeti alivyo navyo bali kwa ujuzi na maarifa aliyonayo yanayoleta tija.
“Chuo chetu cha ‘IJA’ mbadili mtazamo badala ya kutoa ngazi ya cheti ‘certificate’ au stashahada ‘diploma’ muende mbali zaidi kwa kuandaa Programu ya Mafunzo ambayo ndani yake inaweza kuongezwa TEHAMA ili kumpatia mhitimu ujuzi mahsusi ‘basic skills’ kuhusu teknolojia na kumuwezesha kufanya kazi na hata kutatua changamoto yoyote ya kitehama ambayo inaweza kutokea bila msaada wa Wataalam husika,” amesema.
Aliongeza kuwa, ni muhimu Watumishi wa Mahakama wa Kada zote kuwa na uelewa na ujuzi kuhusu matumizi ya TEHAMA hali itakayowezesha Mahakama mtandao ‘e-Judiciary’ kufikika kwa urahisi na haraka zaidi.
“Wengi wetu tunahisi kuwa tunajua kila kitu, lakini asilimia kubwa ya viwango vya elimu tulivyonavyo iwe ngazi ya cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na hata Shahada ya Uzamivu tulisoma wakati ambao maendeleo ya TEHAMA hayajashika kasi, hivyo ni muhimu kukubali kuwa vyeti tulivyonavyo sio kitu kama hatuwezi kwenda sambamba na karne ya 21,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Prof. Juma alibainisha kuwa ujuzi wa teknolojia unamuwezesha mtumishi hata akistaafu kuweza kujiajiri na hata kupata ajira sehemu nyingine katika mashirika mbalimbali na hatimaye kumuwezesha kuendelea kukidhi mahitaji yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alimuahidi Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ili Chuo hicho kiendelee kuwa mfano kwa vingine.
“Mhe. Jaji Mkuu nikuahidi kuwa suala hili tumelichukua, na litafanyiwa kazi hata hivyo Chuo chetu kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kwa Watumishi wa Mahakama hali ambayo imekifanya Chuo hiki kuwa mfano kwa Vyuo vingine na hata nchi nyingine kuja kujifunza jinsi tunavyokiendesha kwa mafanikio,” amesema Mkuu huyo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T).
Akiwa wilayani hapo, Jaji Mkuu pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, vilevile alipokea taarifa ya utendaji wa Mahakama ya wilaya hiyo.
Katika siku ya tatu ya ziara yake, Mhe. Prof. Juma ametembelea na kukagua maendeleo ya shughuli za utoaji haki katika Mahakama ya Wilaya Korogwe ambapo pia alipata fursa ya kuzungumza na Watumishi wa Mahakama hiyo.
Aidha, Jaji Mkuu anatarajia kuhitimisha ziara yake kwa kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Mkinga na hatimaye kufanya majumuisho ya ziara yake kwa kufanya kikao pamoja na Watumishi wote wa Mahakama Kanda ya Tanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto. Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor. Mhe. Prof. Juma ametembelea Mahakama ya Wilaya Lushoto leo tarehe 18 Mei, 2022 ambapo amepata fursa ya kuzungumza na Watumishi wa Chuo hicho pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto pamoja na Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto (hawapo katika picha) leo tarehe 18 Mei, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.
Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Paul Kihwelo akizungumza jambo katika kikao kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Juma na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto pamoja na Watumishi wa Chuo hicho.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Lushoto. Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto. Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe wakimsiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao baada ya kutembelea Mahakama hiyo kwa ziara ya kikazi inayolenga kukagua maendeleo ya shughuli ya utoaji haki nchini katika Kanda ya Tanga.