Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) akisalimiana na Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Zlatan Milisk mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Zlatan Milisk Jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) pamoja na Viongozi wengine wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Zlatan Milisk mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Dodoma.
……………………………………………..
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) leo Mei 18, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Zlatan Milisk Jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Mkenda amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa kwa sasa Wizara inatekeleza agenda ya mageuzi ya elimu kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutaka vijana wanaohitimu kuwa na ujuzi lakini pia kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora.
Ametaja baadhi ya kazi zinazofanyika ili kuleta mageuzi hayo kuwa ni pamoja na kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mitaala.
“Nimefurahi kuona kwamba kuna global support katika hili la mageuzi ya elimu, bahati nzuri hii ya mageuzi ni agenda ya dunia na kwamba Umoja wa Mataifa umeandaa kikao na Wakuu wa Nchi Septemba mwaka huu kujadili mageuzi makubwa ya elimu,” amesema Waziri Mkenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Zlatan Milisk amemuahidi Waziri Mkenda kuendeleza mashirikiano na kuhakikisha malengo ya maboresho kwenye elimu yanatimia ili elimu itolewayo iendelee kuwa bora