Wakazi wa Kata ya Kijiji cha Lundo, kata ya Lipingo wameupongeza uongozi wa Wilaya ya Nyasa, kwa kuwajengea daraja katika daraja la mto Lwika.Daraja hilo linalounganisha, Kitongoji cha zambia na Kijiji cha Lundo na kumaliza kero ya wakazi hao kuliwa na mamba.
Wakazi hao walitoa pongezi wakati wa Ziara ya kamati ya Siasa, ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyasa, walipokuwa wanatembelea na kukagua miradi ya maendeleo, iliyotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa hivi karibuni katika Kata ya Lundo.
Wananchi hao walifafanua kuwa, kwa muda mrefu walikuwa wakishuhudia vifo vinavyotokana na kuliwa na mamba, waliokuwa wakikaa katika mto huo ,na kuwaua wakazi waliokuwa wakivuka kwa kuwa walikuwa wakilazimika kuingia katika mto huo ili wavuke.
Waliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa daraja hakuna kifo chochote cha kuliwa na mamba kilichotokea katika kijiji hicho na wakazi wa kijiji hicho. Wamekuwa wakiishi kwa amani, bila hofu ya kuliwa na mamba katika daraja hilo linalounganisha kitongoji cha Zambia na kijiji cha Lundo.
Ofisa Mtendaji wa kata ya Lipingo, Kuno Ntini alithibitisha daraja hilo ni Ukombozi katika kata yake kwa kuwa kumewafanya wanachi kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Awali walikuwa wakiwa na hofu ya kwenda shamba kwa hofu ya kuliwa na mamba katika daraja hilo lakini kwa sasa wanaendelea vizuri na shughuli za maendeleo.
“daraja hili lilikuwa kikwazo sana kjatika shughuli za kimaendeleo, kwa kuwa watu walikuwa wakishindwa kufanya kazi kwa hofu ya kuliwa na mamba lakini tangu daraja likamilike hakuna kifo cha mamba kilichotokea”
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja hilo, Kaimu meneja wa wakala barabara za mijini na vijijini (TARURA) wilayani hapa Mageta Mteleke ,alisema serikali imetoa Shilingi milioni sabini na tisa nukta nne (79,400,000/=) mpaka kukamilika kwa mradi huu na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Katubu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilayani hapa Abasi Mkweta kwa niaba ya chama hicho Wilayani hapa alipongeza juhudi zilizofanywa na Halmashauri ya kujenga daraja hilo na kuwaomba waendelee kutatua kero za wananchi kwa wakati ili kuwawezesha wananchi hao kupiga hatua za kimaendeleo kwa haraka.
“Napenda kuchukua fursa hii kukupongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Bw.Jimson Mhagama kwa kutekeleza mradi huu ambao ulikuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo katika Kata hii wakazi walikuwa wakiliwa na mamba na hata wananchi wameufurahia sana mradi huu kwa kuwa tangu kukamilika kwake hakuna kifo cha mamba kilichojitokeza katika Daraja hilo” .
Aidha aliwaomba wananchi kutunza miundombinu ya daraja la mto Lwika ili iweze kudumu na kusaidioa vizazi vijavyo.