******************************
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amewaonya baadhi ya watu wanaojihusisha na uhalifu kwenye malori ikiwa pamoja na kujeruhi watu na kuwasababishia majeraha ambapo amesema Jeshi la Polisi limeanzisha doria kwenye barabara kuu na kuwataka madereva kuendelea kuchukua tahadhari.
IGP Sirro amesema hayo leo wakati akifungua Mradi wa Kimkakati wa Fremu 12 za Maduka katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini Dar es salaam, Mradi ambao utawezesha chuo hicho kujiendesha kwenye mahitaji mbalimbali.
Kuhusu Usajili wa Pikipiki (Bodaboda) IGP Sirro amewataka wananchi hasa wanaonunua Pikipiki kwenye makampuni mbalimbali kuhakikisha wanafuata sheria za usajili kwa kuwa na kadi inayoonesha jina halisi la mmiliki wa chombo hicho.
Kuhusu maendeleo ya operesheni ya Panya Road IGP Sirro amesema kuwa, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi imesaidia kudhibiti uhalifu unaotekelezwa na baadhi ya watu/vikundi vya watu na kwamba hadi sasa hali ya nchi ni salama.
Naye Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam SACP Lazaro Mambosasa, amesema chuo hicho kitaweza kujiendesha kutokana na kuwa na miradi mbalimbali ikiwemo bwawa la kufugia samaki pamoja na Mradi mpya wa kimkakati wa fremu 12 za maduka uliogharimu fedha za Kitanzania shilingi milioni 105.