Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Dkt, Mahmoud Abdulwahab akifungua Kikao cha kujadili Mapendekezo ya Muundo mpya wa Taasisi ya Karume katika Ukumbi wa Dkt. Idrisa Muslim Hijja Mbweni Mjini Zanzibar.
Afisa Mwandamizi Uchambuzi, kazi kutoka Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Maulid Shaib Ahmada, akiwasilisha Mapendekezo ya Muundo mpya wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), huko Ukumbi wa Dkt. Idrisa Muslim Hijja Mbweni Mjini Zanzibar
Baadhi ya Wadau waliyoshiriki kikao cha kujadili Mapendekezo ya Muundo wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia zanzibar (KIST), huko Ukumbi wa Dkt. Idrisa Muslim Hijja Mbweni Mjini Zanzibar.
Wadau wa kikao cha kujadili mapendekezo ya muundo wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), wakiwa katika Picha ya pamoja , huko Ukumbi wa Dkt. Idrisa Muslim Hijja Mbweni Mjini Zanziba.
PICHA NA MARYAM KIDIKO – KIST.
**********************
Na Issa Mzee- KIST 16/05/2022.
Wadau wa kikao cha kujadili mapendekezo ya muundo wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia zanzibar (KIST), wamekutana na kufanya kikao cha kujadili mapendekezo ya muundo mpya wa Taasisi hiyo ili kuboresha utendaji na ufanisi wa Taasisi.
Kikao hicho kilichoshirikisha wadau kutoka Taasisi mbalimbali kimefanyika katika ukumbi wa Dkt. Idrisa Muslim Hijja katika Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia (KIST), Mbweni Mjini Zanzibar.
Akizungumza katika ufunguzi Mwenyekiti wa kikao hicho ambae pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Dkt, Mahmoud Abdulwahab amesema lengo la mjadala huo ni kupata maoni, ushauri pamoja na michango mbalimbali ya wadau ili kutengeneza muundo utakao kidhi mahitaji ya Taasisi ya Karume.
Alisema kuwa, endapo muundo mpya utapatikana utaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maeneo mbalimbali ya Tasisi ikiwemo maslahi ya watumishi pamoja na mpangilio mzuri wa majukumu ya watumishi.
“Tumekutana na wadau mbalimbali ili tuweze kuujadili muundo mpya kwa lengo la kuboresha, na kuweka muundo ambao utaendana na wakati kwani Taasisi nyingi hivi sasa zimekuwa zikibadili muundo kwa lengo la kuboresha utendaji, hivyo na sisi tunaamini muundo mpya utaboresha utendaji wetu” alisema Mkurugenzi.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wadau wa kikao hicho kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia (KIST), ili kufikia lengo la kikao hicho pamoja na kuendeleza jitihada za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Mapema akiwasilisha mapendekezo ya muundo mpya wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Afisa mwandamizi Uchambuzi, kazi kutoka Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Maulid Shaib Ahmada amesema muundo unaopendekezwa utawawezesha watumishi kupata maslahi yao kulingana na majukumu, na kuwapa stahiki watumishi wenye dhamana za kimuundo pamoja na kuondoa baadhi ya mambo ambayo husabisha muingiliano wa majukumu katika Taasisi.
“Tunawasilisha sura halisi ya jinsi gani tutaweza kuendeleza majukumu yetu vizuri na kuongeza ubora na ufanisi katika utendaji” alisema Afisa huyo.
Katika muundo huo aliouwasilisha alipendekeza kuwepo kwa idara tisa na vitengo saba vyenye dhamana mbalimbali za kimajukumu ambavyo vilijadiliwa kwa kina na wadau wa kikao hicho na kupatikana mawazo mbalimbali yanayoendelea kufanyiwa kazi.
Alieleza kuwa njia nyingi zimetumika katika kufanya mapitio ya muundo unaopendekezwa ikiwemo kuchambua kwa kina na kupitia majukumu ya msingi ya baadhi ya Taasisi zinazolingana kimajukumu na Taasisi ya Karume.
Aidha alieleza kuwa muundo pendekezwa utamsaidia kwa kiasi kikubwa Mkuu wa Taasisi kupunguza majukumu, kuongeza wigo wa utaalamu kulingana na mahitaji ya Taasisi, pamoja na kurahisisha mtiririko wa mawasiliano katika Taasisi.
Kikao hicho cha kujadili mapendekezo ya muundo mpya wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), kimeshirikisha wadau kutoka Tasisi mbalimbali ikiwemo SUZA, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Afisi ya Rais Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora.
CAPTION.