Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (wa pili kushoto) akiwasili MNH,
wa pili kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Hedwiga Swai.
Wengine ni wajumbe wa Tamati Tendaji ya Chama cha Maafisa Mawasiliano
Serikalini (TAGCO).
Msemaji Mkuu wa Serikali akiwa katika wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi
maalumu (PICU) wenye umri wa siku 30 hadi miaka 14.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya MNH wakimsikiliza Msemaji Mkuu wa
Serikali.
******************
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi ameupongeza Uongozi wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa maboresho makubwa yaliyofanyika
katika utoaji huduma kwa wananchi.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali
akiambatana na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Chama cha Maafisa
Mawasiliano Serikalini (TAGCO) ili kuhamasisha utendaji kazi wa kitengo
cha Habari na Mawasiliano kwa Umma hospitalini hapa.
Katika ziara hiyo Dkt.Abbassi ameridhishwa na utendaji kazi wa kitengo
Habari na Mawasiliano kwa Umma na pia ameupongeza Uongozi wa
Hospitali kwa kutoa ushirikiano mkubwa unaokiwezesha kitengo hicho
kufanya kazi kwa ufanisi.
“Natoa pongezi kwa Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa
Umma, nimemsikia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji anasema Mkuu wa kitengo
hiki anahudhuria vikao vyote vya Menejimenti, Bodi ya Wadhamini na pia
kitengo kinatengewa bajeti ili kufanya kazi na sisi huko nje tunaona utendaji
kazi wake,”amesema Dkt. Abbasi.
Awali akimkaribisha Dkt. Abbasi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt.
Hedwiga Swai, amesema Hospitali imeboresha huduma kwa kiwango
kikubwa ikiwemo kuanzishwa kwa huduma mpya ya upandikizaji figo,
upandikizaji vya kusaidia watoto kusikia na tiba kwa njia ya radiolojia.
Dtk. Swai amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hizo, wagonjwa 47
wamepandakizwa figo, watoto 30 wamepandikizwa vifaa vya kusaidia
kusikia ambapo wananchi 450 wamenufaika na huduma ya tiba radiolojia.
Aidha amesema Hospitali imeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu
ya kutolea huduma ikiwemo kuongeza vitanda vya ICU kutoka 25 hadi
vitanda 80, vumba vya upasuaji kutoka 13 hadi 20, kuongeza mashine za
kusafisha damu kutoka 17 hadi 42 na ununuzi wa mashine za kisasa za
radiolojia ikiwemo CT-Scan na MRI pamoja na kuongeza kiwango
upatikanaji wa dawa kwa asilimi 95.
Dkt. Swai amesema MNH ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya
kuanza kupandikiza ULOTO (bone marrow transplant) kwa wagonjwa
wenye saratani ya damu.
Dkt. Abbasi akishirikiana na Viongozi wa Kamati ya TAGCO, yupo kwenye
ziara maalum ya kutembelea baadhi ya taasisi na idara za Serikali ili
kuangalia hali ya utendaji kazi wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano
Serikalini.