Dar es Salaam. Mashindano ya kuogelea ya FK Blue Marlins yamepangwa kufanyika Jumamosi na Jumapili kwenye bwawa la shule ya kimataifa ya FK iliyopo Bahari Beach jijini.
Meneja wa klabu ya FK Blue Marlins, Opalina Nanyaro amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha waogeleaji kutoka klabu mbalimbali ambapo kila klabu imepewa nafasi ya waogeleaji 30.
Opalia alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na waogeleaji wanafanya mazoezi ili kushindania zawadi mbalimbali siku hiyo.
Alisema kuwa wanatarajia waogeleaji zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Shoppers, Kahawa Cafe, Cool Blue, EFM, Doctors Plaza Polyclinic, PRO Fixers Tanzania, FK International Schools, Viscar Integrated Consulting (TZ) Limited na Coca Cola, GardaWorld.
Kwa mujibu wa Opalina waogeleaji watashindana katika umri tofauti katika staili mbalimbali kwa mujibu wa taratibu. Alisema kuwa pia kutakuwa na mashindano ya waogeaji ya watu wakubwa wenye umri kuanzia miaka 25 na kuendelea au Masters.
Alisema kuwa ‘masters’ wameruhusiwa pia kushindana kwenye kundi la waogeleaji wenye umri wa miaka 15 na zaidi kwa wanawake na kundi la wenye miaka 17 na zaidi kwa wanaume.
Alisema kuwa mbali ya staili tano za kuogelea, waogeleaji hao watahsindanai katika relei ambayo kwa mtindo wa Individual Medley (IM) na Freestyle. Kwenye IM, waogeaji watachanganya staili nne ambazo ni butterfly, backstroke, breaststroke, na freestyle.
“Waogeleaji watakaoshinda katika mashindano hayo watazawadiwa medali na vikombe, tunawaomba wadhamini wajitokeze ili kufanikisha mashindano haya ambayo ni maarufu na yenye mvuto mkubwa,” alisema Opalina.