Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vita Kawawa akikagua Timu ya Young Boys ya kijiji cha Njoomulole kata ya Ligera wilayani Namtumbo kabla ya mchezo wa Fainali ya Bonanza la michezo kati ya Timu hiyo na Kompyuta ya Ligera.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vita kawawa akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Kompyuta ya Ligera kabla ya mchezo wa fainali ya Bonanza la michezo kati ya Timu hiyo na Young Boys ya Njoomlole.
**********************
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
MBUNGE wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Mheshimiwa Vita Kawawa,amewamehimizwa vijana nchini kushiriki michezo ili kuinua vipaji vitakavyoiwezesha Tanzania kupata wachezaji wazuri watakaoliwakilisha vyema Taifa katika michezo mbalimbali.
Mheshimiwa Kawawa,ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akifunga Bonanza la Michezo kwa vijana wa Kata ya Ligera wilayani Namtumbo lililoandaliwa na Chama cha Mapinduzi likiwa na lengo la kuibua vipaji mbalimbali kwa vijana wa kata hiyo.
Alisema,ikiwa vijana wataamua na kujitokeza kushiriki michezo na wazazi watawasimamia vyema watoto wao tangu wakiwa wadogo,basi nchi yetu itapata wachezaji wengi wenye vipaji ambao wataiwakilisha vyema nchi yetu katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Alisema,hata katika nchi zilizopata maendeleo katika michezo zinaonyesha kuwa, wachezaji waliofanya na wanaofanya vizuri hawakuanza ukubwani,bali walianza wakiwa wadogo ndiyo maana zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Alisema,mbali na michezo kuwa ni Burudani, furaha na kuleta amani kwa jamii,lakini kwa sasa michezo ni sehemu ya ajira kwa vijana wengi Duniani.
Ameiomba Serikali na wadau wa michezo hapa nchini, kuwekeza nguvu kubwa kwa watoto wadogo ili kuinua vipaji vyao, badala ya kukimbilia kwa vijana wakubwa ambao tayari wameshaanza kujitegemea.
Katika fainali za Bonanza hilo,Timu ya Kompyuta ya Ligera, iliibuka mshindi baada ya kuifunga Timu ya Young Boys ya Njoomlole kwa Goli 1-0 na kupata zawadi ya mpira mmoja na fedha taslimu Shilingi 50,000 zilizotolewa na Mbunge huyo.