Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini Bi Manyise Mpokigwa akizungumzia kuhusu kutumia Filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio na kuongeza idadi ya watalii kanda ya Kusini.
Jengo la Ofisi za Wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)kanda ya Kusini zilizopo Masasi mkoani Mtwara.
**************************
Na Muhidin Amri,
Masasi
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini, imejipanga kutumia Filamu ya Royal Tour kuendeleza na kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika misitu inayosimamiwa na TFS kwa lengo ka kuvutia watalii na kuleta ajira kwa vijana wa kanda ya Kusini.
Hayo yamesemwa na Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Bi Manyise Mpokigwa wakati akizungumzia walivyojipanga namna watakavyotumia Filamu hiyo iliyozinduliwa wiki iliyopita na Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuongeza mapato ya nchi kupitia sekta ya misitu.
Alisema,Filamu ya Royal Tour imekuja kwa muda muafaka kwani TFS itahakikisha inatumia fursa hiyo kutangaza vivutio na maliasili zinazopatikana katika misitu inayosimamiwa na wakala Kanda ya Kusini kwa ajili ya kuvutia watalii wa ndani na nje ambao watalipa fedha kwa ajili ya kutembelea na kuangalia vivutio na maliasili zilizopo Kanda ya Kusini.
Aidha Kamishina Mpokigwa, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuitangaza Tanzania Kimataifa na imani ya Watanzania Filamu hiyo itaongeza watalii wengi na wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo ya utalii.
Mpokigwa ambaye ni Kamanda wa wakala wa Huduma za misitu(TFS)Kanda ya Kusini alisema, Kanda ya Kusini kuna vivutio vingi,hata hivyo bado havijafahamika sana kutokana na changamoto mbalimbali.
Kwa mujibu wa Kamanda Mpokigwa,TFS kanda ya Kusini ina misitu mitatu ya asili mojawapo ni Msitu wa Londo uliopo katika mkoa wa Lindi,ambako kuna maeneo mazuri ya kupumzika na Mti maarufu wa Nyerere wenye Historia kubwa.
Alisema,mti huo umekuwa kivutio kikubwa tangu ulipogundulika hasa baada ya Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere alipofika na kuchuna gamba la mti huo na kuondoka nalo.
Alisema,kuanzia wakati huo jamii na watu kutoka maeneo mbalimbali wanaendelea kutumia magamba ya mti huo kama tiba na kufanya matambiko ambayo kwa imani zao wanafanikiwa kutokana na shida zinazowakabili.
“sasa mti huo kupitia wakala wa huduma za misitu umewekewa utaratibu maalum ambao kila anayefika katika eneo hilo kwa ajili ya kuchuna magamba analazimika kuchangia kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuchangia mapato ya nchi yetu”alisema.
Mpokigwa,alitaja kivutio kingine ni msitu wa Pindilo uliopo katika wilaya ya Kilwa ambao ni sehemu nzuri kutokana na uwepo uoto wa asili unoafaa kwa ajili ya watu kupumzika.
Pia alisema,katika msitu huo kuna mto Nyange na Bwawa lenye Wanyama aina ya Boko ambao ni walemavu wa ngozi(Albino)wenye uwezo wa kuongea na mtu na ni kivutia kikubwa kwa watu wanaofika katika msituo huo.
Kwa mujibu wa Mpokigwa,katika mkoa wa Ruvuma kuna safu za Milima maarufu ya Matogoro Manispaa ya Songea wenye aina mbalimbali za ndege na ndiyo chanzo cha mto maarufu wa Ruvuma unaotenganisha kati ya Tanzania na Nchi jirani ya Msumbiji.
Alisema, katika milima hiyo kuna maeneo mazuri yanayofaa kwa ajili ya kufanya mikutano mbalimbali kwa kuwa ni sehemu nzuri na tulivu ikilinganisha na maeneo mengine ya katika mkoa huo.
Alitaja Msitu mwingine ni Mwombesi(Mwombesi Nature Reserve) unaopatikana katika wilaya ya Tunduru wenye Wanyama wengi mchanganyiko kama vile Tembo,Nyati, Swala,Paka pori, Fisi,Nyoka na maporomokoya asili.
Alisema,Msitu wa Mwombesi ni hifadhi iliyo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Msumbuji kupitia Mto Ruvuma na mwaka 2021 watalii zaidi ya 50 kutoka Mataifa mbalimbali walitembelea katika msituo huo na kufanya mkutano.
Alisema,kwa sasa kazi kubwa inayofanyika ni kuboresha mazingira hasa ya miundombinu ya barabara ili Watanzania na watalii kutoka nje ya nchi waweze kufika katika msituo huo.