Profesa Issa ShivjiMhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM akizungumza katika kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa BoT.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga akifungua kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa BoT.
…………………………………..
NA MWANDISHI WETU
MWANAZUONI Profesa Issa Shivji amewataka vijana kusoma kitabu cha Wasifu wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwani watajifunza mambo mengi na mazuri ya kuwajenga katika kupambania Tanzania wanayoitaka.
Prof. Shivji ambaye ni mmoja wa waandshi wa kitabu hicho chenya majuzuu matatu ametoa kauli hiyo leo Mei 5 jijini Dar es Salaam katika kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumzia kitabu hicho Prof. Shivji amesema kuwa mapambano ya uhuru enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa ni hatua ya kwanza na kwamba mapambano bado hayajakwisha katika kuipata Tanzania tunayoitaka.
“Kwanza niseme tu mapambano ya uhuru, ilikuwa ni hatua ya kwanza kabisa, na mapambano bado hayajakwisha. Kwa sababu uhuru bado haujakamilika, kwahiyo mapambano bado yanaendelea na ndiyo maana tukasema katika kuandika wasifu huo wa Mwalimu jambo ambalo tulilojalibu kuonesha ni stori yenyewe miaka 60 tangu uhuru imekuwa ni historia ya mapambano ya wananchi na Watu wa Tanzania wakiongozwa na Mwalimu,” amesema Prof. Shivji na kuongeza kuwa,
“Sasa kwa upande wangu nawasihi sana vijana wasome huo wasifu ili wasione kwamba mambo mazuri tunayotaka, nchi tunayotaka hatutaipata kama zawadi bali itapatikana kwa mapambano,”.
Prof. Shivji amesema anamanisha kwamba sio wengi wetu watafaidika na hayo mapambano, lakini hata hivyo lazima watu wapambane ili vizazi vijavyo vifaidike na wapate nchi tunayotaka.
Akizungumzia kuhusu taasisi za fedha husun BoT kuandaa kongamano kama hilo la masuala ya kisiasa badala ya masuala ya fedha ama uchumi amesema ni mwanzo mzuri kwani huwezi kutenganisha Sekta ya Fedha na mambo mengine.
“Kama alivyosema Gavana mwenyewe huwezi ukatenganisha Sekta ya Fedha na mambo mengine, hali halisi ya nchi na huwezi ukatenganisha Sekta ya Fedha bila kujua historia,” ameeleza Prof. Shivji.
Amesema kongamano hilo pamoja na kwamba limejikita kwenye wasifu wa Mwalimu Nyerere, lakini wasifu na historia ya Mwalimu kwa Tanzania inawafunza Watanzania mambo mengi.
“Kama nilivyogusia katika mchango wangu kuna mambo ya Sekta ya Fedha kwa mfano tulipoyataifisha mabenki. Hivyo leo tunahitaji kujua yaliyotokea na jinsi haya mabenki walivyopambana mpaka yakasalimu amri,” ameongeza.
Amesema kipindi cha Mwalimu Nyerere ubishani kati yake na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) unatoa funzo hadi sasa kwani alikuwa akipinga namna shirika hilo lilivyotaka kutumia fursa ya kuyumba kwa uchumi kuifanya Tanzania ibadili misimamo yake.
Kwamba hadi leo mashirika kama hayo yanye nguvu ya kifedha yamekuwa yakishinikiza Taifa kama la Tanzania kubadili misimamo ambayo ni kwa maslahi ya nchi.
“Kwa sababu bado wanaendelea kututawala kwa njia moja ama nyingine,”.
Kwa upande wake Gavana wa BoT Profesa Florens Luoga amesema kwamba wameandaa kongamano hilo ili kutoa fursa ya kutambulishwa kwa vitabu vya wasifu wa Mwalimu Nyerere.
“Wakati Rais anavizindua hivi vitabu kule Kibaha, hivi vitabu vilikuwa havijatambulisha, wananchi wengi walikuwa tu wanaona yale majuzuu matatu. Lakini kwa kawaida unapoona majuzuu kama yale mtu wa kawaida inampa uzito kidogo kusema anunue asome.
“Lakini ukivitambulisha wananchi wanajua nini kilichomo na nini kinaweza kikapatikana kutoka katika hivyo vitabu,”.
Ameongeza kwamba BoT iliona iandae kongamano hilo ikiwa ni sehemu ya jitihada zake katika kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Ameeleza kuwa BoT kwa namna ya pekee imekuwa ikihakikisha kuwa inamuenzi Mwalimu Nyerere kwanza kwa kuweka ufadhili wa masomo kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa viajana ambao wengi wao wana uwezo wa kuendelea kulihudumia Taifa kupitia BoT ama kupitia taasisi nyingine za umma.
“Ndio maana unaona kuna vijana wamekaa pale, wengine wako katika masomo ya uchumi, wengine wapo katika masomo ya sayansi,”.
Aidha amesema vile vile ilikuwa ni nafasi kwa ajili ya kuujulisha umma kuhusu mfuko wa ufadhili wa masomo ya Mwalimu Nyerere ambao unasimamiwa na BoT.
Mwandishi wa vitabu na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya akizugumza katika kongamano hilo hku akionesha moja ya vitabu vilivyochapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota.
Mwandishi wa vitabu Profesa Saida Yahya Othman akifafanua jambo wakati akizungumza katika kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa BoT.
Mwandishi wa Vitabu Profesa Ng’wanzi Kamata akielezea namna mwalimu alivyotoroshwa katika moja ya vitendo vya Uasi vilivyowahi kutokea wakati Baba wa Taifa Mwalimu J.K.Nyerere akiongoza nchi na jinsi Oscar Kambona alivyoshiriki kutuliza uasi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Comminication Bw. Bakari Machumu akishiriki katika Kongamano hilo.
Manaibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kushoto ni Ndugu Julian Banzi RAPHAEL Dk. Bernard Kibese wakifuatilia mijadala katika kongamano hilo.
Kaimu Meneja Uhusiano kwa Umma na Itifaki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi.Vicky Msina akifuatilia mijadala katika Kongamano hilo llilofanyika leo kwenye ukumbi wa BoT.
Picha mbalimbali zikionesha Washiriki mbalimbali wa Kongamano hilo wakiwa katika Kongamano.