****************************
04/05/2022 DAR ES SALAAM
Siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Hamad Masauni kutoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuwakamata Panya road, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro ametoa salamu kwa kikundi hicho cha Panya road kuacha kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani nakwamba Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na watu hao.
IGP Sirro amesema hayo wakati alipofanya ziara katika Kata ya Kunduchi Mtongani na Kata ya Kawe jijini Dar es salaam na kuwapa pole watu waliojeruhiwa na kikundi hicho cha panya road.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kawe Askofu Josephat Gwajima amesema, wananchi wanahaki ya kulaumu Jeshi la Polisi ili liweze kutimiza wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na mali zao na pia wananchi wanawajibu wa kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili matukio ya namna hiyo yasijirudie.
Aidha, IGP Sirro amesema ni vyema wazazi na walezi wakaimalisha malezi ya familia zao pamoja na kushiriki kwenye vikundi vya ulinzi shirikishi.
Naye mmoja kati ya wananchi wa Kata ya Kunduchi Bi. Sophia Ali amesema ni vyema viongozi wa serikali ya mtaa kuandaa utaratibu maalum wa vikao vya mara kwa mara vitakavyowezesha wananchi kuwataja watu wanaojihusisha na uhalifu kwa kupiga kura ya siri.