Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vita Kawawa akishiriki ujenzi wa kituo cha Afya Ligera wilayani Namtumbo ambapo Serikali imetoa kiasi cha Sh.milioni 250 za awali kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakapokamilika kitahudumia wakazi wa kata ya Ligera na maeneo ya jirani.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa kulia,akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Ligera Simon Komba baada ya kumaliza kukagua ujenzi wa kituo cha Afya kinachojengwa katika kijiji hicho.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ligera kata ya Ligera baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Ligera ambapo amewataka kuwa walinzi wa vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya ujenzi na miundombinu yake.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa wa pili kushoto akimsikiliza Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ligera Dkt Abel Godson baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Ligera.
Mkazi wa kijiji cha Ligera wilayani Namtumbo Haluna Tindwa(70) ambaye ni mlemavu wa miguu akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vita Kawawa wa pili kushoto akiwaongoza wakazi wa kijiji cha Ligera kwenda kushiriki ujenzi wa kituo cha Afya baada ya Serikali ya awamu ya sita kutoa Sh.milioni 250 kwa ajili ya kujenga kituo hicho ambacho kitahudumia wananchi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa akizungumza na baadhi ya watoto wa kijiji cha Ligera wilayani Namtumbo baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Ligera ambapo amewataka watoto hao kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Picha zote na Muhidin Amri
…………………………………………….
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
MBUNGE wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Mheshimiwa Vita Kawawa,amewataka watumishi wa Serikali wanaopewa kazi ya kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo kuwa wazalendo na waadilifu badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Kawawa ametoa kauli hiyo jana, baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Ligera wilaya Namtumbo kinachojengwa kwa lengo la kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa kata hiyo.
Alisema, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kusikia kilio cha wananchi wa kata hiyo kuhusiana na changamoto ya huduma ya afya imetoa Sh.milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho cha Afya.
Kawawa amemshukuru Rais Samia, kwa kutoa fedha hizo ambazo zitatumika kumaliza kero ya ukosefu wa huduma za Afya kwa wananchi wa kata ya Ligera ambao kwa sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu hadi kata ya Mkongo au Hospitali ya wilaya Namtumbo mjini kufuata matibabu.
“hapa Ligera hakuna kituo cha Afya mnalazimika kwenda maeneo mengine kufuata matibabu,leo nasimama mbele yenu kumshukuru sana Rais wetu mpendwa na Serikali kutupatia Sh.milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha Afya katika kata yetu”alisema Kawawa.
Amewataka mafundi na wasimamizi wa ujenzi huo,kuhakikisha wanakuwa waadilifu wa fedha zilizoletwa na kutozidisha gharama za bei ya vifaa kwani jambo hilo linaweza kuchelewesha kazi hiyo.
Amewaasa wananchi kutoa ushirikiano na kushiriki kwa karibu katika ujenzi wa kituo hicho pamoja na kuwa walinzi wa vifaa vinavyoletwa ili mradi huo ukamilike haraka.
Aidha alisema, Serikali imetoa Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya Magazini ambacho ujenzi wake unaendelea vizuri,Sh. milioni 600 kujenga Shule ya Sekondari Msisima na Sh.bilioni 4 zitakazotumika kujenga shule ya Sekondari ya Wasichana katika eneo la Migelegele.
Alisema,Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuifungua wilaya ya Namtumbo kwa kujenga miundombinu na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wake.
Kawawa,amewaomba wananchi wa Ligera na Namtumbo kwa ujumla kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi na kuwaomba kuiamini Serikali yao.
Katika hatua nyingine,Kawawa amewakumbusha wananchi wa kata hiyo na Jimbo la Namtumbo kujiandaa na kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi linatalotarajia kufanyika Mwezi Agosti Mwaka huu.
Alisema, zoezi hilo ni muhimu kwa kila mtu kushiriki kwani lisaidia Serikali kujua idadi ya wananchi ili iweze kupanga mipango yake ya maendeleo kulingana na idadi kamili ya watu wake.
“Zoezi la sensa ya watu na makazi litafanyika mwezi Agosti Mwaka huu,nawaomba sana wananchi wa Jimbo langu la Namtumbo tutoe ushirikiano mkubwa kwa kushiriki zoezi hilo ambalo lina manufaa makubwa,msiwawasikilize hata kidogo baadhi ya watu watakaokuja na kuwapotosha”alisema.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ligera na Njomulole wameishukuru serikali kujenga kituo cha Afya,na kueleza kuwa kitakapo kamilika kitamaliza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma za afya.
Macelina Mapunda alisema, katika kijiji cha Ligera kuna Zahanati ndogo iliyojengwa miaka mingi,hata hivyo baadhi ya huduma zikiwamo za upasuaji hazipatikani kutokana na ukosefu wa vifaa tiba na Wahudumu wenye sifa.
Ameiomba Serikali kupitia kamati ya ujenzi,kuharakisha ujenzi wa kituo cha Afya ili waweze kupata huduma muhimu karibu na maeneo yao kwa kuwa sababu zahanati hiyo haiwezi kutoa baadhi ya huduma kama ya upasuaji.