Na Joachim Mushi, Igunga
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Elimu). Mhe. David Silinde amefunga rasmi shughuli za Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa, yaliyokuwa yakifanyika wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, huku akisisitiza Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu ukiwemo Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) kuboresha elimu nchini.
Naibu Waziri Mhe. Silinde ametoa kauli hiyo alipokuwa akifunga rasmi shughuli za Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa kwa mwaka 2022, zilizokuwa zikifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Akizungumza katika hafla hiyo, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa elimu ndio maana imeridhia utoaji wa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne, ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu pasipo na ubaguzi.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu pia Serikali inajenga shule za washichana za mikoa kwa mikoa yote nchini na kwa mwaka wa fedha 2021/22 tayari Serikali imetoa fedha za ujenzi wa sekondari kwa mikoa 10, na kila shule moja inatarajiwa kugharimu Shilingi bilioni 4.
“…Kwa mwaka wa fedha 2022/23 kupitia bajeti ya TAMISEMI Serikali imetenga tena fedha nyingine katika mikoa 10 kugharamia ujenzi wa shule hizo za sekondari. Na kama hiyo haitoshi Serikali imetenga fedha katika kata 232 ambapo kwa awali kila kata imepatiwa shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari, na katika bajeti mpya Serikali itapeleka fedha nyingine katika kata 234 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari,” alisisitiza Naibu Waziri Mhe. David Silinde kwa wadau wa elimu.
Aidha alibainisha kuwa Serikali pia imeondoa vikwazo kwa watoto wa kike ambao walikuwa wameacha shule kwa sababu mbalimbali ili warejee na kuendelea na masomo yao, jambo ambalo linaaishiria viongozi wanatambua umuhimu wa elimu kwa jamii na kuhakikisha inamfukia kila mmoja pasipo na vikwazo.
Vijana wa Skauti wakiongoza maandamano ya wanafunzi kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu.
|
Baadhi ya wanafunzi wa Msingi na Sekondari wakiwa kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa, yaliyofanyika wilayani Igunga Mkoa wa Tabora. |
Hata hivyo aliongeza kuwa Serikali imepeleka fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia fedha maarufu za ‘Rais Mama Samia’ kujenga miundombinu na tayari imejenga vyumba vya madarasa elfu kumi na tano vyenye thamani ya shilingi bilioni 3oo, ambayo madarasa hayo yameanza kutumia sehemu mbalimbali.
“Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, ili kupunguza changamoto za wanafunzi hao wanapopata masomo yao, tunashukuru nyinyi wadau asasi za kiraia kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita,” alibainisha Naibu Waziri huyo.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania, Ms. Faraja Nyalandu alisema baada ya wanachama wa TEN/MET kutembelea shule anuai na wilayani hapo na kuzungumza na wanafunzi, walimu, wanajamii kuhamasisha elimu na kupata maoni yao, wameishauri Serikali kuongeza bajeti ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule za Msingi ili kukabiliana na limbikizo la wanafunzi katika darasa moja.
Aidha wameshauri Jamii iendelee kuhamasishwa kuthamini elimu katika suala zima la kuchangia nguvu kazi na rasilimali hasa chakula cha watoto wawapo shuleni na pia kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi.
“…Ipo haja ya kuongeza ajira za walimu ili kuendana na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa hasa kwa shule za msingi, Ipo haja ya wanajamii na watendaji kuthamini taaluma ya walimu na kujiepusha kutoa lugha zisizo na staha kwa walimu. Walimu wa madarasa ya KKK kujengewa uwezo zaidi ili kuweza kuwafundisha watoto lugha ya kiswahili na kwa wale wanaoandaliwa kuingia darasa la kwanza…Serikali iangalie uwezekanao wa kuwapata walimu wazuri wa lugha ya kiingereza ili kuboresha ujifunzaji wa lugha.
Ipo haja ya Serikali kufanya utambuzi wa kipekee kwa watoto wenye ulemavu wanaofanya vizuri kulingana na hali zao na aina ya ulemavu walionao, pia walimu wao watambulike na kupewa tuzo kama walimu wengine.
Maadhimisho ya Juma la Elimu kwa mwaka huu yalijumuisha wadau wa elimu kwa uratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuchangia uboreshaji wa elimu nchini. Pia kuhamasisha na kukumbusha jamii, serikali, mashirika yasiyoya kiserikali na wadau mbalimbali wa elimu umuhimu wa uchangiaji wa elimu kwa kuzingatia kauli mbiu isemayo: Gharamia Elimu Bora Kuboresha Matokeo ya Ujifunzaji: Elimu Kwanza.