*************************
Tarehe 25 Aprili, Timu ya Ushauri wa Kielimu ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam (EducationUSA) ilikutana na wanafunzi 70 wa Kitanzania waliorejea kutoka Ukraine baada ya masomo yao kukatishwa na uvamizi wa Urusi.
Wanafunzi hao wa shahada ya kwanza wanatafuta fursa ya kuendelea na masomo yao nchini Marekani.
Walifahamishwa kuhusu uwezekano wa kusaidiwa na EducationUSA – ambayo ni kitengo ndani ya Ubalozi kinachowasaidia wanafunzi mahiri wa Kitanzania kujiunga na elimu ya juu nchini Marekani.
Mkutano huu ulifunguliwa rasmi na Afisa wa Masuala ya Umma wa Ubalozi wa Marekani James Rodriguez ambaye alichangia uzoefu wake wa kuwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza nchini Marekani na maisha yake akiwa mfanyakazi wa kujitolewa wa Peace Corps nchini Ukraine miaka michache iliyopita.
Katika mkutano huo, Afisa wa Uhamiaji Bi Christa Divis aliwafahamisha wanafunzi hao kuhusu taratibu za uombaji viza za Marekani.
Aidha, Mwanafunzi wa Kitanzania anayesoma Chuo Kikuu Connectcut nchini Marekani Bilis Kalolela, kwa njia ya mtandao , alielezea hatua alizopitia katika kutuma maombi yake hadi kujiunga na elimu ya juu nchini Marekani.
Mwanafunzi mwingine, Bi. Florida Rwejuna ambaye anatarajia kujiunga na Michigan state university alielezea jinsi alivyoweza kupata ufadhili wa masomo kutoka chuo hicho.
Zaidi ya hayo, Afisa wa Kitengo cha Biashara cha Ubalozi Bw. Lupatu Athanaus alikutana na Wakala wa Elimu uliowasaidia vijana hao kwenda nchini Ukraine ili kujadili fursa za ushirikiano.
Mkutano huu uliwapa wanafunzi hawa ari na hamasa kubwa wanapoelekea kuanza kuandaa maombi yao ya kujiunga na vyuo vya Marekani.