*************************
Mwandishi wetu Babati
MDAU wa maendeleo wa Mkoa wa Manyara, Emmanuel Khambay amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya thamani ya shilingi milioni 10.280 kwenye hospitali ya Mji wa Babati (Mrara) vituo vitatu vya afya na zahanati mbili.
Msaada huo umehusisha meza za kuhifadhi dawa na vyakula vya wagonjwa, mabenchi ya kukalia wagonjwa na viti vya kukalia manesi na madaktari.
Khambay amesema ametoa msaada huo baada ya kuguswa aliposikia kuna changamoto ya vifaa hivyo.
Amesema vifaa hivyo vitaganywa kwenye hospital ya Mrara ya mji wa Babati, vituo vya afya Mutuka, Singe, Bonga na zahanati za Nakwa na Malangi.
“Baada ya viongozi wa UVCCM mji wa Babati wakiongozwa na Mwenyekiti Hassan Mdinku na katibu hamasa Idd Sulle kusema changamoto hizo nilitoa kidogo nilichonacho ili kupungua changamoto hizo,” amesema Khambay.
Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange amewapongeza UVCCM Babati mjini kwa kuwa wabunifu na kutafuta wadau kama Khambay wanaoweza kumaliza au kupunguza changamoto.
“Wangekuwa wengine wangekuja kwangu kulizungumzia lakini ninyi mmekuwa wabunifu mmeona tatizo mkamtafuta mdau wa maendeleo Khambay na akatoa msaada huo,” amesema Twange.
Amesema suala hilo atalisema popote kwani UVCCM Babati mjini wamekuwa watafiti na kutafuta majawabu hivyo jumuiya nyingine waige mfano huo kwa kutatua changamoto kwa vitendo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya vijana wa CCM (UVCCM) mji wa Babati, Hassan Mdinku amesema baada ya kuona changamoto kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati hizo waliwafuata wadau mbalimbali wa maendeleo ili kutatua mapungufu hayo.
“Tunamshukuru mdau wetu wa maendeleo Khambay kwa kutuunga mkono kwenye changamoto hizi ambazo kwa kiasi fulani zitamaliza au kupunguza mapungufu yaliyopo,” amesema Mdinku.