OR-TAMISEMI
Mkurugenzi wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe , Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Ntuli Kapologwe ameitaka Timu ya usimamizi wa shughuli za Afya (CHMT) katika Mikoa yote Tanzania bara kuimarisha usimamizi wa fedha za dawa walizopokea kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Amesema fedha hizo zisimamiwe ipasavyo ili hizo zitumike katika kuboresha upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ya afya lakini pia zitumike kukuza mtaji utaotumika katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Dkt. Ntuli ametoa kauli hiyo Mkoani Kigoma April 25,2022 wakati wa ukaguzi shirikishi Mkoani humo na ambapo Mkoa huyo ulipokea Shilingi Bil 2.7 kutoka Serikali kuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajiki ya ununuzi wa dawa.
“Fedha hizo ni Revolving Fund inatakiwa kuzunguka na Shilingi Bil. 2.7 ni fedha nyingi mno kwa Mkoa mmoja, CHMT niwaombe hakikisheni mnasimamia kikamilifu fedha hizi ili tuondokane na madeni ya dawa lakini pia zikizungushwa vizuri tutapata faida ya mtaji ambao utaendelea kuboresha utoaji wa huduma ya afya”Amesema Ntuli.
Aidha amewataka Makatibu afya na Waganga Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia stahiki za watumishi wa Idara ya afya ikiwemo stahiki ya kupandishwa madaraja ili kuleta motisha na kuongeza tija katika utendaji kazi.
“ Lazima tuwatengenezee mazingira mazuri watu ambao tunafanya nao kazi ili kuwaongezea ari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kutoa huduma kwa wananchi” Amesema Ntuli
Pia ameishauri CHMT kutembelea na kuimarisha usimamizi katika utekelezaji wa mindombinu ya kutolea huduma za afya huku ikizingatia ushirikiano katika uandaaji wa taarifa za utekelezaji wa miundombinu hiyo.
Aidha Ntuli amempongeza Mganga Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Waganga Wakuu wa Wilaya katika kuwatambua watu wenye ulemavu wapatao 16,088 katika Mkoa wa Kigoma na kuunda kamati 491 za watu wenye uemavu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba ameahidi kushirikiana na CHMT katika kushughulia mapungufu yaiyobainishwa katika kikao hicho ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya katika Mkoa wa Kigoma.