Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na ujumbe wa Tanzania aliombana nao katika ziara yake ya kikazi inayoendelea Jumhuri ya Korea. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Togolani Edriss Mavura baada ya kumkabidhi kifungashio chenye maudhui ya kutangaza Utalii wa Tanzania katika Ofisi za Ubalozi jijini Seoul, Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo Kiku cha Wanawake cha EWHA (EWHA Womans University) walipotembelea Chou hicho kilichopo jijini Seoul, Korea.
………………………………….
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameanza zaira ya kikazi katika Jamhuri ya Korea. Ziara hii ya siku tano inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 29 Aprili 2022.
Ziara hii sambamba na kuboresha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, inalenga kujadili na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa buluu, usafirishaji na uchukuzi, utamaduni na sanaa, teknolojia, elimu na biashara.
Waziri Mulamula akiwa nchini Korea, kwa nyakati tofauti anatarajia kuonana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri wa Mambo Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-Yong, Wanadiplomasia, viongozi wa Taasisi za Elimu na Mafunzo na Jumuiya ya Diapora.
Vilevile, Waziri Mulamula akiwa jijini Seoul, Korea anatarajiwa kushiriki katika hafla ya siku ya maadhimisho ya Miaka 58 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka tarehe 26 Aprili.
Sambamba na hilo Waziri Mulamula atashiriki kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea yatakofanyika jijini Seoul tarehe 29 Aprili 2022.
Waziri Mulamula katika ziara hii ameambatana na Watendaji mbalimbali wa Serikali akiwemo Dkt. Aboud S. Jumbe Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Balozi Caesar C.Waitara Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Magese Emmanuel Bulayi Mkurugezi wa Idara ya Uvuvi katika Wizara ya Uvuvi na Mhandisi Aaron Kisaka Mkurugenzi wa Idara ya Usafirishaji katika Wizara ya Uchukuzi na Ushafirishaji.