Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene (wa kwanza kutoka kulia), Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi na Afisa Mkuu wa Mkaguzi wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa (kushoto) wakati wa Futari iliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson akizungumza wakati wa hafla ya kufuturisha wabunge iliyoandaliwa na Benki ya NMB katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB – Filbert Mponzi akizungumza wakati wa hafla ya kufuturisha Jijini Dodoma.
………………………………..
Katika mwendelezo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Benki ya NMB iliandaa Futari iliyohudhuriwa na Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa Dini mbalimbali, Uongozi wa NMB na baadhi ya wateja katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 500, ambapo mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Spika ameipongeza na kuishukuru NMB kwa kuandaa hafla hiyo ya Ibada iliyowakutanisha kwa upendo, imani na kuendeleza uhusiano mwema kati ya benki hiyo na Muhimili wa Bunge.
Akizungumza kwa niaba ya NMB, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara – Filbert Mponzi alisema “Kwa kuandaa futari hii, sisi kama NMB tunaendelea kudumisha ukaribu na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na wateja wetu. Huu ni wakati mzuri kwa ndugu zetu Waislamu na jamii kwa ujumla kutafakari juu ya upendo kwa familia zetu, shukrani kwa Mungu na toba za dhati”
Mponzi alibainisha kuwa hiyo ndio sababu ya NMB kuipa umuhimu mkubwa jambo hilo na wamekuwa wakifanya hivyo toka miaka ya nyuma- Kwa mwaka huu, tayari wameshatoa futari kwa mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma na baadaye watafanya hivyo Visiwani Zanzibar.