Na Dotto Mwaibale, Ikungi
WANANCHI wa Kijiji cha Mwisi Kata ya Lighwa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametakiwa kutunza chakula ili kujikinga na baa la njaa litakaloweza kutokea siku za usoni.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa wakati akiwahutubia Wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara wa kuzungumzia maendeleo na kupokea kero za wananchi ili zifanyiwe kazi ulioandaliwa na Diwani wa Kata hiyo Gabriel Mukhandi na kuhudhuriwa na umati wa watu.
“Ndugu zangu mwaka huu haukuwa na mvua za kutosha na kusababisha mazao shambani kuwa machache hivyo nawaombeni tunzeni chakula kwani kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula” alisema Likapakapa.
Akijibu baadhi ya kero zilizoibuliwa na wananchi katika mkutano huo kama kukosekana kwa jengo la Mama na Mtoto alisema wananchi wanapaswa kuanzisha ujenzi hadi ngazi ya boma na Serikali isasaidia kulimalizia.
Akizungumzia Bwawa lililokuwa la TASAF ambalo hivi sasa limeharibika alisema litafanyiwa ukarabati ili lirudi katika hali yake ya kawaida na wananchi wawezekunufaika nalo lakini akaomba baada ya ukarabati huo iundwe kamati maalumu itakayokuwa ikisimamia bwawa hilo ambalo lilikuwa likitumika kwa kilimo cha umwagiliaji na uvugaji wa samaki.
Pia Likapakapa aliwaomba wananchi wa kata hiyo kutenga maeneo kutoka kwenye mashamba yao kwa ajili ya miundombinu ya barabara zitakazoweza kuwasaidia panapotokea matukio ya dharura kama magonjwa, moto na wajawazito waweze kufikiwa kwa urahisi na vyombo vya usafiri.
Halikadharika Likapakapa akizungumzia masuala ya kutumia muda mwingi katika maziko baada ya mtu kufariki ambapo alisema suala hilo ni la kijamii zaidi wenye maamuzi ni mfiwa hama viongozi wa dini wanaoongoza ibada za mazishi na Serikali haiwezi kuingilia jambo hilo kwani ni la kiimani zaidi.
“Hatuwezi kuingilia suala ili kwani wenye maamuzi ni ndugu wa mfiwa husika kwani wengine wanakuwa wanawasubiri ndugu zao wanaoishi mbali na viongozi wa dini hawezi kupangiwa muda wa kufanya ibada za mazishi” alisema Likapakapa.
Likapakapa aliyasema hayo kufuatia swali lililouklizwa na mmoja wa wananchi akiomba Serikali kupanga muda wakati wa shughuli za mazishi baada ya kuonekana yanatumia muda mwingi hadi kufikia wananchi wengine kuondoka katika misiba kwa kuchoka kutokana na kuwepo kwa mlolongo wa mambo mengi.
Diwani wa Kata hiyo Gabriel Mukhandi alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuzungumzia ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Kijiji cha Mwisi ambalo ni muhimu sana na kuwa litakuwa likiwahudumia wananchi kutoka kata za Ntuntu, Misughaa, Makiungu na Munghaa.
Alitaja lengo lingine kuwa ni kuzungumzia ukarabati wa Bwawa la TASAF ambalo lilisombwa na mafuriko, umaliziaji wa nyumba ya walimu katika Sekondari ya Lighwa ambao boma lake limedumu kwa zaidi ya miaka tisa pasipo kukamilika na pia walizungumzia zoezi la kitaifa la Anwani za makazi na postikodi.
Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Stamili Dendego alisema mikutano ya namna hiyo ni ya muhimu sana wananchi kushiriki ili waweze kutoa kero zao na kuchukuliwa na wahusika ziweze kutafutiwa ufumbuzi ambapo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria kwenye mkutano huo.
Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya hiyo Pius Sanka aliwaomba wananchi wa kijiji hicho na kata hiyo kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ambazo tayari zipo kwenye maeneo yao kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa ndani ambao mchakato wake umeanza.
Katika mkutano huo viongozi wanne kutoka vyama vya Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na TLP wa kijiji hicho walivihama vyama vyao na kujiunga CCM viongozi hao ambao walikabidhi kadi zao ni Patrick Suna, Swalehe Hamadi, Anisia Kisiu na Thomas Misanga.