Timu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) (kushoto) wakkiwavuta Tume ya Utuimishi wa Walimu kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume wa michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Timu ya Uchukuzi SC (kushoto) wakiwavuta Hazina kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume wa michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mfungaji Kalova Kihwele wa timu ya Uchukuzi akidaka mpira kutoka kwa Mary Kajigili ( C), huku Eveline Edwin ( C ) wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) akijaribu kuupoka bila mafanikio katika mchezo wa netiboli uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri ambapo Uchukuzi wameshinda kwa magoli 43-17.
***************************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya netiboli ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) imeendeleza wimbi ya ushindi kwa kuwafunga Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa magoli 43-17, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Uchukuzi iliyoshinda michezo yake yote mitatu ya kwenye kundi na kujihakikishia kuingia hatua ya nane bora, walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 18-9.
Katika mchezo mwingine timu ya Wizara ya Afya ilizinduka na na kuwafgunga Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwa magoli 26-1. Afya walikuwa na magoli 11-8 hadi mapumziko; nao Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) waliwachapa Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kwa magoli 27-21. Hadi mapumziko TPDC walikuwa wakiongoza kwa magoli 11-8.
Kwa upande wa wanawake timu ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Roads waliwavuta Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa 2-0; huku Idara ya Mahakama wakiwaadabisha ndugu zao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa 2-0; wakati Wizara ya Afya wakiwavuta Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa 2-0; huku NCAA wakiwavuta Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa 2-0; nao TPDC waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa 2-0 na TAMISEMI waliwaliza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa 2-0.
Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume timu ya Uchukuzi iliwavuta Hazina kwa mivuto 2-0; nao Wizara ya Maliasili na Utalii waliwavuta Wizara ya Afya kwa 2-0; huku Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliwavuta Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwa 2-0; wakati Wizara ya Mambo ya Ndani waliwacheza kwata Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa 2-0; huku Wizara ya Kilimo iliwavuta Tume ya Utumishi wa Walimu kwa 2-0; na timu ya Idara ya Mahakama ilipata ushindi wa chee baada ya Shirika la Umeme nchini kutoonekana uwanjani.
Kwa upande wa mchezo wa soka timu za Kongwa DC na Wizara ya Nishati zilitoka sare ya bao 1-1. Bao la Kongwa lilifungwa na Johnson Joel na la Nishati lilifungwa na Charles Kitundu.
Wakati huo huo, wanariadha takribani 40 kutoka kwenye timu mbalimbali zinazoshiriki kwenye mashindano ya kuwania Kombe la Mei Mosi leo watafukuza upepo katika mbio za mita mbalimbali zitakazofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Wanariadha hao kwa upande wa wanaume na wanawake watakimbia mita 100, 200, 400, 800, 1,500, 3,000, kupokezana vijini mita 100×4 na kurusha tufe.