**********************
NA WAF-DODOMA
Imeelezwa kuwa ugonjwa wa kisukari umeendelea kuwaathiri watanzania wengi ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya watanzania milioni 60 kuna watanzania milioni 5.8 wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za kinga Dkt. Omary Ubuguyu wakati wa uzinduzi wa mpango wa kuzuia ulemavu wa kutokuona unaoweza kuletwa na madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye macho utakaotekelezwa kanda ya kati uliofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Dkt. Ubuguyu amesema madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye macho yamekua yakiongezeka na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia pazia la jicho (retina) na kuathiri uoni siku hadi siku bila kuwa na dalili.
“Tanzania inakadiriwa kuwa takriban asilimia 5.7 ya watu wenye umri wa miaka 20 hadi 79 wana ugonjwa wa kisukari. Tafiti zilizofanyika hapa nchini zimeonyesha kuwa asilimia 35 ya watu wenye kisukari wana madhara ya ugonjwa huo kwenye macho na asilimia 1 ya watu hao hupata ulemavu wa kutokuona au uoni hafifu”. Amesema Dkt. Ubuguyu.
Aidha, Dkt. Ubuguyu amesema kuna mikakati tofauti ya kuzuia ulemavu wa kutokuona unaosabababishwa na madhara ya ugonjwa wa kisukari kwenye retina ikiwa ni pamoja kuanza uchunguzi kwa ‘Diabetic Retinopathy’ kwa wale walio na kisukari pia kuzingatia tiba na ushauri unaotolewa na wataalam ikiwemo kubadili mtindo wa Maisha.
Naye Meneja Mpango wa huduma za macho Wizara ya Afya Dkt. Bernadetha Shilio amesema kwa ufadhili wa shirika la afya duniani (WHO) mwaka 2015 Tanzania iliendesha zoezi la tathmini ya huduma kwa wagonjwa wa kisukari na huduma za macho kwa wagonjwa wenye madhara ya kisukari kwenye macho.
Dkt. Shilio amesema tathmini hiyo ilionyesha asilimia 30 tu ya wagonjwa wa kisukari walifikiwa na huduma za uchunguzi wa macho huku sababu ikitajwa kuwa ni upungufu kwenye utaalamu, vifaa na vifaa tiba, eneo la kutolea huduma za uchunguzi pamoja na kutokuwepo kwa muongozo wa uchunguzi na tiba.
Katika uzinduzi wa mpango huo Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikabidhiwa kamera maalum ya uchunguzi wa madhara ya kisukari kwenye retina ya macho kutoka kwa Dkt. Rosemary Brennan ambaye ni Daktari bingwa mshauri wa macho kutoka Hospitali ya Raimore Scotland.