Mkuu wa Wilaya ya Nyasa akiongea na wananchi katika kijiji cha Lituhi Wilkayani Nyasa na Picha Nyingine akikabidhi Mikataba ya ujenzi wa Miradi ya Maji katika Kata za Lituhi na Liuli Wilayani Nyasa
**************************
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Nyasa imetambulisha miradi mikubwa 2 yenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 11.3 itakayotatua Upatikanaji wa maji safi na Salama katika Kata 4 za Lituhi, Mbaha, Liuli na Kihagara Wilayani hapa.
Miradi hiyo imetambulishwa katika mikutano ya Hadhara yenye lengo la kuwashirikisha wananchi, ili waweze kushirikiana na Mkandarasi atakayetekeleza Mradi, na Mkutano iliyofanyika katika Kata ya Lituhi na Liuli na kuhudhuririwa na wananchi na Viongozi wa Chama na Serikali.
Akizungumza katika Mikutano, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kanali Laban Thomas, amemtaka Mkandarasi anayetekeleza Mradi, kuhakikisha anajenga mradi kwa ubora na kwa wakati na kuhakikisha maji yanatoka, na kuwa Mradi endelevu kwa kuwa Serikali inalengo la kutatua kero ya maji, hivyo fedha za Serikali ziendane na thamani halisi ya Mradi. Pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika Mradi na kulinda na kutunza Vyanzo vya maji.
“Ninakutaka Mkandarasi utakayetekeleza Mradi huu kuhakikisha kuwa unajenga kwa ubora na maji yanatoka, na kuwa mradi endelevu kwa kuwa Serikali inalenga kutatua kero ya maji, hivyo fedha za Serikali ziendane na thamani halisi ya Mradi nitakuja kukagua. Pia ninawataka wananchi kutoa ushirikiano wa ujenzi wa Mradi huu na kulinda na kutunza vyanzo vya maji”.
Awali akitoa Taarifa ya Miradi hiyo Kaimu Meneja wa RUWASA Wilayani Nyasa JeremiahMaduhu amesema, wamejipanga kimkakati kusimamia na kutekeleza miradi hiyo ili iweze kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
Amevitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi katika Kata ya Lituhi ni Lituhi,Kihuru,Nkaya, na Mwela mpya na Katika Kata ya Mbaha ni Mbaha,Ndumbi na Liweta na Katika Mradi Mwingine wa Liuli Vijiji vitakavyonufaika ni Nkalachi,Hongi Mkali A na Mkali B.
Ameongeza kuwa shughuli zitakazofanyika ni Ujenzi wa vyanzo vyanzo vya maji,ukarabati wa Matanki na Ujenzi wa Matenki mapya,ununuzi wa Bomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji na Miradi hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia.Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Mkandarasi anayetekeleza mradi huu kwa kuwa anaanza mara moja baada ya kutambulishwa.
Wananchi wa Kata Hizo wameipongeza Serikali kwa, kutatua changamoto ya maji kitika kata zao kwa kuwa awali walikuwa na Miradi ambayo ilijengwa zamani na miundombinu yake ilikuwa imechakaa, hivyo wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa Ndugu Jimson Mhagama kwa kutatua Changamoto mbalimbali katika Wilaya ya Nyasa.
NB.Anayezungumza wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kanali Laban Thomas na wa pili ni kaimu Meneja Ruwasa Mhandisi Jeremia Maduhu.