Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Mwenda, akiwaongoza watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, kwenda kuona michoro ya miambani Kondoa Irangi, Dodoma.
Muhifadhi na Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Kondoa Irangi, Bw. Zuberi Mabie, akitoa maelezo kwa watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, waliotembelea michoro ya miambani Kondoa Irangi, Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, wakiwa na furaha wakati wa ziara yao kwenye michoro ya miambani Kondoa Irangi, Dodoma.
Eneo ambalo hutumiwa kufanya matambiko katika miamba ya Irangi Kondoa, ambapo watu hulazimika kutambaa chini ya mwamba kwenda kuzungumza na miungu.
****************************
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea maeneo yenye hadhi ya urithi wa Dunia ikiwemo michoro ya miambani ya Irangi Kondoa Mkoani Dodoma ili kujua historia ya nchi na Serikali inavyohifadhi mali kale kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lusius Mwenda, wakati wa ziara ya utalii wa ndani wa watumishi 40 wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Zanzibar katika michoro ya miambani Irangi Kondoa Mkoani Dodoma.
Bw. Mwenda alisema lengo la ziara hiyo ni watumishi waliotoka Zanzibar pamoja na mambo mengine ni kujua fursa za utalii zilizopo Tanzania Bara na kuwa mabalozi kwa wengine wa mali kale adimu nchini.
Kwa upande wake Muhifadhi na Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Kondoa Irangi, Bw. Zuberi Mabie, alisema kuwa michoro ya miambani iliyopo Irangi Kondoa ni miongoni mwa hifadhi za mali kale zilizoingizwa katika hadhi ya urithi wa Dunia mwaka 2006 chini ya Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Alisema maeneo hayo ya mali kale yana manufaa makubwa kiuchumi kwa kuwa yanatoa fursa za ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambayo mapato hayo yanaenda pia kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.
Bw. Mabie, amewapongeza watumishi hao kutoka Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kutembelea michoro hiyo na kujionea jitihada za Serikali za kuihifadhi na kuwataka watumishi hao kuwa sehemu ya kuhifadhi maeneo hayo muhimu.
Naye Mtumishi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Bi. Saada Said Seif, alishukuru kwa kupata fursa ya kuona michoro hiyo ambayo alikiri imemvutia na kuwaomba wananchi wengine hususani kutoka Zanzibar wafanye utalii wa ndani wa kwenda kuangalia michoro hiyo.
Michoro ya miambani Kondoa yenye rangi nyeupe, nyekundu na nyeusi inasadikiwa kuchorwa na Wawindaji na waokota matunda hasa wa kabila la Wasandawe miaka 1500 mpaka 50,000 iliyopita huku michoro ya rangi nyekundu ikidhaniwa kuwa ya muda mrefu zaidi.
Maeneo mengine yaliyoingizwa kwenye urithi wa Dunia chini ya UNESCO ni pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, hifadhi ya Serengeti, hifadhi ya mlima Kilimanjaro, magofu ya Kilwa na Songo mnara na pori la akiba la Selous.