Mshambuliaji Geofrey Mugope (12) wa timu ya Hospital ya Benjamin Mkapa (12) akipiga mpira huku Masoud Hamad wa Hazina akijaribu kuuwahi mpira huo kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Shell Complex jijini Dodoma. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Mfungaji Joverda Prosper (Mwenye soksi za njano) wa timu ya Wizara ya Madini akitafuta mpira katikati ya walinzi Caroline Gwau na Husna Ahmed wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika mchezo wa netiboli wa michuano ya kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Madini waliibuka kidedea kwa magoli 26-13.
*************************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU za Wizara, Taasisi za Umma na makampuni binafsi za michezo ya netiboli na soka zimetunishiana misuli kwa kufungana magoli katika mashindano ya Kombe la Mei Mosi, iliyofanyika kwenye viwanja vya Jamhuri na Shell Complex.
Katika michezo ya netiboli timu ya Uchukuzi SC iliwachaka Mzinga kwa kuwafunga magoli 49-5, ambapo washindi waliweza kuongoza kipindi kwanza wakiwa mbele kwa magoli 25-1. Mfungaji mahiri wa Uchukuzi SC, Neema Rusan alifunga magoli 44 huku Bahati Herman akichangia magoli matano.
Katika mchezo mwingine timu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), waliwafunga Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa magoli 42-14. Hadi mapumziko Tanesco iliyokuwa ikiongozwa na mfungaji wake Neema Mbuja walikuwa mbele kwa magoli 22-4.
Nayo timu ya Hospital ya Benjamin Mkapa waliwapa dozi Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kwa kuwafunga magoli 14-11. Hatahivyo, pamoja na mechi hii kuwa na ushindani mkubwa timu hizo zilikwenda mapumziko zote zikiwa na magoli 6-6.
Katika michezo mingine timu ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) waliwachabanga Wizara ya Afya kwa magoli 37-10. TRA walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 17-7; nayo timu ya Wizara ya Madini waliwaliza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa magoli 26-13. Madini waliongoza nusu ya kwanza kwa magoli 14-8.
Hatahivyo, timu ya Wizara ya Nishati ilipata ushindi wa chee wa magoli 40 na pointi mbili, baada ya wapinzania wao Wizara ya Mambo ya Ndani kuchelewa kufika kiwanjani; halikadhalika Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) walipata ushindi wa magoli 40 na pointi mbili baada ya Wizara ya Maji kuchelewa kufika.
Kwa upande wa mchezo wa soka timu ya TANROADS waliwafunga Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa magoli 2-1. Magoli ya washindi yalifungwa na Zebedayo Mwalim na Yohana Mpakaliro huku la NCAA lilifungwa na Aidan Frank.
Nayo timu Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) walitoka sare na Hazina kwa kufungana bao 1-1. Bao la Hazina lilifungwa kwa njia ya penalti na Salim Suleiman Bakari wakati aliyeisawazishia BMH alikuwa ni John Bwire.; nayo timu ya TAMISEMI ilipata ushindi wa chee baada ya wapinzani wao Mashtaka kuchelewa kufika kiwanjani.
Michuano hii inayotarajiwa kufunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka tarehe 20 April, 2022 inaendelea leo kwa mechi za michezo ya netiboli na soka kwenye viwanja vya Jamhuri, Shell Complex, Cental Sekondari.