*******************
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge amewataka Madiwani wa Chalinze Kuwa sehemu ya kushirikiana na wataalamu na watendaji wa Halmashauri kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuinua Pato la Halmashauri.
Aidha amewaasa kuwa viongozi wa kujifunza kutoka kwa wengine ili kuwa na weledi wa kuweza kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao.
Alitoa rai hiyo wakati, akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani katika utendaji kazi kama wawakilishi wa wananchi katika mamlaka za serikali za mitaa, katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze.
Kunenge aliwataka madiwani kwa kushirikiana na watendaji kuibua vyanzo vipya vya mapato na siyo kubaki na vyanzo vya zamani, “hivyo kama madiwani mnatakiwa kuwa na ufahamu wa sheria ili kufanya maamuzi sahihi katika vikao na kuwa wabunifu katika kuiendeleza halmashauri.” Mkuu wa Mkoa alisema.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Afisa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ,Bwana Rashid Baghdellah akitoa mada mbalimbali katika mafunzo hayo aliwataka madiwani kujua wajibu wao kama wawakilishi wa wananchi katika mamlaka za serikali za mitaa na kuisimamia halmashauri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo .
“Fuatilieni upimaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika ngazi ya Halmashauri,Usimamizi wa Ujasiriamali na Fursa katika Mazingira mnakoishi waheshimiwa Madiwani.”
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisisitiza ushirikiano baina ya madiwani na watendaji wa Halmashauri.
Pia aliwataka kujitafakari kiushindani wa kuinua mapato ya halmashauri nchini ili kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.
Ridhiwani aliwataka madiwani wasijihusishe kupanga safu wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
“Wanachama waje kupimwa kwa sifa zao, mwenye sifa ya uongozi na si Bora kiongozi lakini sio muwe sehemu ya kujihusisha na mambo ya kupanga safu”alieleza Ridhiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye pia ni Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Hassan Mwinyikondo, ameishukuru Halmashauri yake kupitia Mkurugenzi Mtendaji kwa kuandaa mafunzo ya kuwawezesha madiwani katika utendaji wa shughuli zao kama wawakilishi wa wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.”
Hakika kupitia mafunzo haya kama madiwani tumejengewa uwezo na hakika tumebadilika na tutaisimamia halmashauri kwa kuzingatia sheria,taratibu na kanuni ili kuwaletea wananchi maendeleo.” alieleza Mwinyikondo
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo katika uendeshaji wa masuala mbalimbali ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi sahihi ya fedha za serikali katika mamlaka za serikali za mitaa.