Mratibu wa mpango wa Taifa wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Arusha ,Helena Materu akizungumza katika hafla hiyo jijini Arusha .(Happy Lazaro)
…………………………………………
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mkoani Arusha bado vipo juu ,hivyo elimu zaidi inatakiwa kutolewa kuhakikisha jamii inaepukana na vitendo hivyo.
Aidha takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa ,kwa mkoa wa Arusha jumla ya wanawake 4,510 walifanyiwa ukatili wa kijinsia, huku kati ya hao mabinti wakiwa ni zaidi ya 1000 wenye umri chini ya miaka 18 .
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mratibu wa mpango wa Taifa wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Arusha,Helena Materu wakati akizungumza katika tamasha la uelimishaji katika ngazi ya jamii kuhusu ndoa za utotoni,na kupinga ukatili wa kijinsia na ukeketaji lililoandaliwa na shirika la DSW Tanzania lililofanyika katika kata ya Musa halmashauri ya Arusha dc .
Materu amesema kuwa,takwimu hizo kwa mkoa wa Arusha bado zipo juu kutokana na jamii kuendelea kufanya vitendo hivyo ikiwemo ukeketaji kwa watoto ambao unafanywa kwa siri pindi watoto wanapozaliwa ambapo aliitaka jamii kuungana kwa pamoja katika kupinga vitendo hivyo na hatimaye takwimu hizo ziweze kushuka ifikapo 2023.
“Tunashukuru sana shirika hili la DSW kwa namna ambayo limekuwa likitoa elimu kwa jamii na wasichana wadogo kuhusu maswala ya ndoa za utotoni na ukeketaji ambapo kupitia watoto hao waliopata elimu hiyo wameweza kuwa mabalozi wazuri wa kuwafundisha wenzao ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo hivyo katika jamii zao ,kwa kweli huo ni mfano mzuri wa kuigwa kwani wanaisaidia serikali kwa kiasi kikubwa”amesema Materu.
Mkurugenzi wa Shirika la maendeleo na afya kwa vijana DSW Tanzania,Peter Owaga amesema kuwa,shirika hilo linatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo wa Binti na maendeleo ambao unatekelezwa katika halmashauri ya Arusha dc katika kata tano ikiwemo ya Musa ambapo jamii imeweza kujengewa uwezo kuhusu maswala ya ukatili ,ndoa za utotoni na ukeketaji lengo likiwa ni kuhakikisha jamii na mabinti wanakuwa na uelewa wa kutosha na kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo hivyo.
Peter amesema kuwa,kata hiyo imekuwa mfano wa kuigwa ambapo wataendelea kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za vijana ikiwemo ukarabati wa maktaba ndogo iliyotolewa na halmashauri hiyo wakishirikiana na kata kwa lengo la kusaidia vijana na mabinti kupata sehemu ya kujifunzia.
Afisa miradi wa shirika hilo,Juliana Mndanga amesema kuwa,mradi huo wa Binti na maendeleo unalenga kupinga ukatili wa kijinsia hususani ukeketaji katika kata hizo ambapo umeleta manufaa makubwa sana kwa jamii na mabinti kwa ujumla.
Amesema kuwa,mradi huo unalenga kuwafikia mabinti walioko ndani ya shule na nje ya mfumo usio wa shule ambapo zaidi ya mabinti 1000 wamefikiwa na elimu mbalimbali ikiwemo maswala ya Afya ya uzazi,stadi za kazi,ukatili wa kijinsia na ukeketaji ambapo waliopo nje ya mfumo wamefikiwa na elimu ya ujasiriamali.
Baadhi ya wananchi ,wakizungumza katika tamasha hilo,Janeth Laizer waliomba kuwepo kwa sheria kali za kuwabana watu wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili ikiwemo kufungwa jela ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikifanywa kwa siri.