MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameihoji serikali mkakati ilionao wa kujenga nyumba za Walimu katika Halmashauri ya Ikungi ili kupunguza changamoto iliyopo.
“Kwa sababu walimu wetu wanafanya kazi nzuri na tuliwajengea madarasa mazuri huko vijijini ambakowanatakiwa wakae karibu,Je ni mkakati upi wa haraka wa kutafuta fedha za kutosha kuweza kumaliza tatizo hilo ambalo ni kubwa na linapunguza ari ya walimu kufanya kazi,?amehoji Mtaturu.
Akijibu swali hilo April 13,2022,Bungeni Jijini Dodoma,Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),David Silinde amesema serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya nyumba za walimu Nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya Ikungi.
Amesema Ikungi ina mahitaji ya nyumba 454 na nyumba zilizopo ni 172, ambapo ili kukabiliana na upungufu uliopo kwa mwaka wa fedha 2022/2023,Halmashauri ya Wilaya Ikungi imetenga Shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za Walimu katika shule za Mandigu Kata ya Munga, Nali Kata ya Siuyu, Mankumbi Kata ya Kikio na Mau Kata ya Ikungi.
“Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu kwa Halmashauri ikiwemo na Halmashauri ya Ikungi kadri fedha zitakavyopatikana,”alisema Silinde.
Amekiri kutambua changamoto hizo na kwamba fedha zilizotolewa katika Halmashauri hiyo ni ndogo.
Ametaja mkakati wa serikali ni kuhakikisha kila sekondari mpya inayojengwa inaenda sambamba na ujenzi wa nyumba za walimu ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Lakini pia tuna mikakati mingi ikiwemo kutafuta fedha na jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunamaliza kwanza ujenzi wa madarasa na shule katika maeneo yote yenye uhitaji na mara baada ya kumaliza hiyo hatua yetu ya pili ni kujenga nyumba kwa walimu hususan katika mazingira yale magumu,
Katika swali lingine la nyongeza Mtaturu ametaka kujua mkakati wa serikali wa kuongeza idadi ya walimu katika Halmashauri ya Ikungi.
“Na kwa sababu serikali imetangaza ajira za walimu ,na kwa kuwa halmashauri ya Ikungi ina upungufu mkubwa,Je ni lini serikali itahakikisha kwamba inaongeza idadi ya walimu ambao wapo katika halmashauri ya Ikungi?,
Akijibu swali hilo Silinde amemuhakikishia mbunge huyo kupitia ajira za walimu zilizotangazwa watawapeleka wengine katika Halmashauri hiyo.
“Nimuhakikishie mheshimiwa mbunge katika hatua ambazo sisi tumeshatangaza ajira,sisi TAMISEMI tutaajiri walimu 9,800 na katika nafasi hizo za ajira tutakazoajiri sehemu ya ajira tutapeleka katika halamshauri ya Ikungi,”amesema Silinde.