Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini akizungumza kwenye Mahafali ya Kumi na Nne ya Kuhitimu Kidato cha Sita cha Mwaka 2022 katika Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo leo Aprili 12, 2022 iliyopo Kata ya Busegwe, Wilaya ya Butiama Mkoani, Mara.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini ambaye ni Mgeni Rasmi kwenye Mahafali ya Kumi na Nne ya Kuhitimu Kidato cha Sita cha Mwaka 2022 ya Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo iliyopo Kata ya Busegwe,Wilaya ya Butiama, Mkoani Mara, akikabidhi vyeti vya uongozi bora kwa baadhi ya wanafunzi wa Shule hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wahitimu wa Kidato cha Sita cha Mwaka 2022 wa Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo leo Aprili 12, 2022 kwenye Mahafali ya Kumi na Nne ya Kuhitimu Kidato cha Sita katika Shule hiyo iliyopo Kata ya Busegwe, Wilaya ya Butiama Mkoani, Mara.
……………………………………..
Na Mwandishi wa MoHA.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini amewataka wanafunzi wahitimu wa Kidato cha Sita mwaka huu, kujiepusha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuwapelekea kuwa wateja wa Jeshi la Polisi.
Akizungumza na wanafunzi wahitimu wa kidato cha sita waliopo shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo, amewataka kutii Sheria na maadili ya Kitanzania na kuepuka kujihusisha katika utumiaji wa madawa ya kulevya na mauaji.
“Niwaombeni mkirudi nyumbani baada ya kumaliza kidato cha sita mtii Sheria na kufuata maadili ya Tanzania”
Naibu Waziri Sagini amesema hayo leo Aprili 12, 2022 katika Mahafali ya Kumi na Nne ya Kuhitimu Kidato cha Sita Mwaka 2022 katika Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo iliyopo Kata ya Busegwe, Wilaya ya Butiama Mkoani, Mara.
Akiwakumbusha kuhusu Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yanayoadhimishwa tarehe 13 Aprili mwaka huu wilaya ya Butiama, Naibu Waziri huyo, aliwapongeza wanafunzi wahitimu wa Kidato cha Sita wa Mwaka 2022 kwa kuonyesha kwa vitendo ushiriki wao wa kupambana na adui ‘ujinga’ ambaye ni moja ya maadui watatu wa Nchi yetu Tanzania yaliyobainisha na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“Mwalimu Nyerere alibainisha wazi maadui watatu wa Nchi yetu ambao ni Maradhi, Umaskini na Ujinga. Wakati wa Utawala wake aliongoza watanzania kupigana na maadui hao bila kuchoka”. Alisema.
Akitoa Salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Wahitimu wa Kidato cha Sita, Walimu pamoja na Wageni waalikwa kwenye Mahafali hayo,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Sagini amemshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha Sekta ya elimu katika Wilaya ya Butiama kwa kupitisha na kuwezesha miradi mbalimbali ya Elimu inayoendelea katika jimbo lake.
Hata hivyo Mbunge huyo wa Jimbo la Butiama amewataka Wanafunzi wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari kuendeleza ubunifu wao na kuwasisitiza wahamasishe wazazi na walezi wao kushiriki kwenye Sensa ya Makaza itakayoanza Agosti mwaka huu 2022.