Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Mashaka Sinkala akielezea hatua waliyofikia kwenye Mradi wa Maji Amani Makoro.
Mwananchi wa Kijiji cha Amani Makoro Grace William akielezea furaha aliyonayo kwa Serikali kuwapelekea mradi wa maji.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Mashaka Sinkala akionyesha hatua waliyofikia kwenye Mradi wa Maji Amani Makoro.
Muonekano wa tenki la maji linalojengwa katika kijiji cha Amani Makoro wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kupitia fedha za Ustawi.
…………………………………………………….
Selemani Msuya, Mbinga
BAADA ya kupita miaka 40 ya kutumia maji ya visima na mto, Mei mwaka huu wanakijiji 5,022 wa Kijiji cha Amani Makoro na Mkeke kata ya Amani Makoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wanatarajia kuchota maji bombani.
Matarajio hayo ya wanakijiji hao, yanasababishwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Wilaya ya Mbinga ambao wanatekeleza mradi wa maji kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Meneja wa Ruwasa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Mhandisi Mashaka Sinkala amesema wilaya hiyo imepata fedha za Uviko-19 Sh.899.9 ambapo Mradi wa Maji Amani Makoro umetengewa Sh.479.6.
Sinkala amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ametengewa Sh.milioni 380 na fedha nyingine zinatumika kununua mabomba ambayo yatasambazwa kwa urefu wa kilomita 22.8 ambapo hadi sasa wameshasambaza mabomba kilomita 12.
Mhandisi Sinkala amesema kazi nyingine zinazofanyika katika ujenzi huu ni ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita zaidi ya 100,000, mitaro, kulaza mabomba, kujenga uzio na vituo vya kuchotea maji.
“Mradi wa Maji Amani Makoro hadi sasa umefikia asilimia 60 na tunatarajia kuwa utakamilika Mei 15 mwaka huu na utanufaisha watu 5,022 wa vijiji vya Amani Makoro, Mkeke na Kitongoji cha Mkeso cha kata ya Lutumbandosi,” amesema.
Meneja huyo wa Ruwasa amesema pamoja na kunufaisha watu zaidi 5,000 pia watapeleka maji kwenye bandari kavu za makaa yam awe zilizopo kijijini hapo na taasisi za umma kama shule, zahanati na nyingine.
Amesema utekelezaji wa mradi huo umekumbana na changamoto mbalimbali kama mvua na nyingine ila wamefanikiwa kuidhibiti na matarajio yao ni mradi kukamilika kama ambavyo wamepanga.
Aidha, meneja huyo amesema Wilaya ya Mbinga katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepatiwa Sh.bilioni 2.5 ambazo zinatumika kutekeleza miradi 12, ikiwemo hiyo ya Uviko-19.
“Hapa tunatekeleza mradi wa Tanga, Amani Makoro, Mabuni, Utiri, Kitanda, Ifakara, Myangayanga, Ruwaita, Ruhagara, Kihuruku na Kitai ambapo ikamilika tutafikia asilimia 71 na lengo la 2025 kufikia asilimia 85 litatimia,” amesema.
Meneja huyo amesema ujio wa Ruwasa umekuwa mkombozi mkubwa katika sekta hiyo ya maji na kwamba matumaini yao ni kuhakikisha maji vijijini yanapatikana kwa asilimia 100.
Ofisa Tarafa ya Kigonsera Focus Mgeni, amesema kinachofanywa na Serikali kuwapatia wananchi maji ni cha kupongezwa na wao watalinda miradi hiyo kwa nguvu kubwa.
“Sisi kama tarafa tutahakikisha miundombinu na vyanzo vya maji hapa Mbinga vinalindwa ili fedha ambazo zinatumika kujenga miradi hii inakuwa endelevu,” amesema.
Mtendaji wa kata ya Amani Makoro Joachim Kaponda amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwaona wananchi hao baada ya miaka 40 ya kuomba kupatiwa maji.
Kaponda amesema ukosefu wa maji ya uhakika kijijini hapo shughuli nyingi za maendeleo zilizorota, hivyo wanaamini kwa sasa kasi ya maendeleo itapatikana.
Nao wakina mama wa Amani Makoro, Rose Samweli, Hilda Komba na Grace William wamesema wao kama wakina mama wanamshukuru Rais Samia kuwakomboa kupitia maji kwani changamoto hiyo ilikuwa inakwamishwa shughuli za maendeleo.
Wakina mama hao wamesema ujio wa maji hao utachochea ufaulu wa wanafunzi kuongezeka, kwa kuwa watatumia muda mwingi kusoma na sio kutafuta maji.
Aidha, wamesema matumaini yao ni kuona magonjwa ya milipuko yanapungua kama sio kuisha kabisa, huku wakiahidi kuilinda miundombinu ya miradi hiyo.
“Kabla ya mradi huu hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa shida, hali ambayo ilichangia wao kutumia muda mwingi kutafuta maji, hivyo kukosa usingizi, watoto kuchelewa shule, kilimo na biashara zilizotota. Nasema Rais Samia ameupiga mwingi kwa kutuletea Ruwasa,” amesema Rose.