Baadhi ya wakazi wa kata ya Ruvuma katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakisubiri kupata huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu inayotolewa bure na wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo Shirika la MDH na Amref Health Africa.
Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii(CHW)wakiwasikiliza baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma ya uchunguzi wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo inayotolewa bure na wizara ya Afya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa.
Muhudumu wa Afya ngazi ya jamii9CHW) kata ya Ruvuma katika Manispaa ya Songea Aziza Kivina kulia,akimsikiliza mkazi wa mtaa wa Mibulani Hadija Mohamed aliyefika kupata huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya kupambana na ugonjwa wa TB inayolenga kuibua na kuwaanzishia dawa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo.
Wahudumu wa ngazi ya jamii(CHW) kata ya Bombambili wakiendelea na majukumu ya kuhudumia wananchi wakati wa kampeni hiyo.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Melikebu kata ya Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa wataalam wa afya.
……………………………………….
Na Muhidin Amri,
Songea
KAMATI ya usimamizi wa Huduma za Afya ya mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa, imeanza Kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wanaoishi katika mazingira duni na hatarishi.
Maeneo hayo ni kata ya Ruvuma na Bombambili katika Manispaa ya Songea,ambayo yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza jana,Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala alisema,kampeni hiyo imehusisha kata hizo kutokana na wakazi wake wengi kuishi kwenye makazi duni ambayo ni hatarishi na rahisi kupata ugonjwa huo.
Alisema,moja ya makundi hatarishi yaliyoko katika hatari ya kupata maambukizi ya kifua kikuu ni umaskini katika jamii ikiwamo kuishi chumba kimoja watu wengi,nyumba zisizokuwa na mwanga na hewa ya kutosha.
Alisema, ndiyo maana Serikali ya mkoa kupitia wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na wadau wa mandeleo Shirika la MDH na Amref Afrika imedhamiria kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035.
Kwa mujibu wa Dkt Mbawala ni kwamba,katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa wameanza kwenda kila wilaya kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo ili jamii iweze kufahamu na kuchukua hatua ya haraka ikiwamo kuwahi Hospitali kupata matibabu.
Dkt Mbawala alisema, kampeni hiyo itafanyika katika wilaya zote za mkoa huo na matumaini kuwa italeta tija kubwa na itasaidia kuokoa maisha ya watu ambao wameambukizwa ugonjwa huo lakini wameshindwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali.
Dkt Mbawala alieleza kuwa,ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na muhimu kwa mtu aliyepata ugonjwa huo kuwahi haraka ili kuepuka vifo na kuambukiza wengine.
“Serikali yetu ya mkoa wa Ruvuma inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwamo MDH- Amref Health Africa katika kuboresha huduma za afya ili kwa pamoja tuweze kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2035”alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Manispaa ya Songea Dkt Emanuel Kiwale alisema, hali ya maambukizi ya kifua kikuu katika manispaa ya Songea ni makubwa ambapo amezitaja kata zinazoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu ni Ruvuma na Bombambili.
Dkt Kiwale alisema, hali hiyo inachangiwa sana na umaskini kwa wakazi wake ambapo wanalazimika kuishi watu wengi katika chumba au nyumba moja isiyokuwa na mwanga au hewa ya kutosha.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Ruvuma,wameipongeza Serikali kupeleka huduma ya uchunguzi katika maeneo yao kwani itasaidia sana kuokoa maisha ya watu wengi hasa wazee ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma.
Hadija Ismaila alisema,kuna watu wanasumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu lakini wameshindwa kwenda kupata matibabu kwenye vituo na Hospitali kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo nauli ya kutoka nyumbani hadi Hospitali.
Alisema,badala yake wanaendelea kuteseka na hata wapo waliopoteza maisha na kuiomba Serikali na wadau wa afya kuhakikisha wanasogeza huduma zake karibu na wananchi badala ya huduma hizo kupatikana makao makuu ya kata,wilaya na mkoa.
Ibrahim Salum alisema,huduma hiyo ni nzuri kwani inatoa majawabu ya shida za wananchi wenye maradhi ambao wana tabia ya kumeza dawa bila kupata ushauri wa Madaktari.
Amewapongeza watoa huduma kwa kazi wanaofanya ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi,na kuwataka kuendelea kuwasaidia watu ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha ikiwamo maradhi ya mara kwa mara.