Baadhi ya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO 19
Baadhi ya wanafunzi wakionekana na furaha mara baada ya kutoka darasani
………………………………………………….
Na Zillipa Joseph, Katavi
Halmashauri ya Wilaya ya Mlele ni moja ya Halmashauri tano zinazounda mkoa wa Katavi. Halmashauri hii kama zilivyo halmashauri zote hapa nchini nayo ilipokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele Theresia Irafay, kwa mwaka 2021-2022 Halmashauri ya Mlele ilipokea kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni ishirini na tisa, mia mbili ishirini elfu, na mia tatu hamsini kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 27 na ukamilishaji wa maboma 20 ya vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali.
Aidha katika fedha za UVIKO-19 ambazo ni shilingi milioni mia nne themanini (480,000,000/-) halmashauri ilweza kujenga vyumba vya madarasa 24 katika vituo shikizi 6 ambavyo pia vimefanikiwa kusajiliwa na kuwa shule za msingi kamili.
Shule hizo ni pamoja na Ulyambogo, Izenga, Imalauduki, Utende, Kamwelwe na Mlogolo.
Halmashauri ya Mlele pia imefanikiwa kuandikisha wanafunzi 1,915 wa darasa la awali sawa na asilimia 78.6 ambapo wavulana ni 929 na wasichana ni 990.
Kwa upande wa darasa la kwanza walioandikishwa ni 4,117 sawa na asilimia 152.71 ambapo wavulana ni 2,092 na wasichana 2,025.
Hali hii inaelezwa kuwa moja ya mafanikio serikali iliyofikia baada ya kujenga shule nzuri zinazovutia wananchi kupeleka watoto wao shule.
Mwanaisha Ali ni mkazi wa kijiji cha Mlogolo, alisema kwa mwaka huu amepeleka watoto wake wawili kuanza shule.
‘Ninaishukuru serikali kwa kweli wametuletea shule karibu na pia madarasa yenyewe yanavutia, madawati yapo watoto hawakai chini’ alisema.
Nae Masanja Kibua mkazi wa kijiji cha Utende ameshauri wazazi wenzie hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni kuukataa ujinga na kuwapeleka watoto wao shule kwani elimu inatolewa bure.
Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na iliyokuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (ambayo sasa ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wananwake na Makundi Maalum) wa mwaka 2021 Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kujumisha elimu ya awali katika elimu ya msingi kupitia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 kwa kuzitaka shule zote za msingi kuwa na darasa la awali.
Ni ukweli kwamba kuwepo kwa mazingira rafiki ya kisera kumepelekea kuwepo kwa ongezeko la uandikishaji wa ananfunzi wa darasa la awali kufikia 500,000 ndani ya mwaka mmoja kutoka 1,069,823 mwaka 2015 hadi 1,562,770 mwaka 2016 kwa nchi nzima.
Hata hivyo bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu hasa katika shule hizo za awali ambapo serikali inashauriwa kuongeza ajira zaidi ili wanafunzi hawa wapate kile wanachostahili.