**********************
Leo tarehe 07/04/2022 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Jerry C. Muro amesimamia tukio la kihistoria la uwekaji saini ya makubaliano ya kufanikisha uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 3 katika sekta ya kilimo cha alizeti katika wilaya ya ikungi
Makubaliano hayo ni uwekezaji katika sekta ya kilimo cha alizeti baina ya halmashauri ya ikungi na kampuni ya kimataifa ya uwekezaji ya Alfardaws ambayo itawekeza katika kilimo cha alizeti, ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti , pamoja na kilimo cha mbegu za alizeti ambazo zitauzwa hapa nchini na nje ya nchi
Katika makubaliano haya halmashauri itahakikisha inafanikisha upatikanaji wa ardhi hekari 1,700 ambazo zitatolewa kwa mwekezaji kwa makubaliano ya kuwalipa fidia wananchi ambao ardhi yao itachukuliwa kwa ajili ya uwekezaji huu ambapo zaidi ya shilingi milioni 246 zimetengwa
” Nichukue nafasi hii kipekee kuwashukuru sana wawekezaji wa Alfardaws ltd kwa kuamua kuwekeza ikungi, kituo cha uwekezaji Tanzania TIC kanda ya kati, mkurugenzi wa halmashauri ya ikungi Justice kijazi pamoja na wakuu wa idara za kilimo, ardhi, na sheria kwa kufanikisha kukamilika kwa makubaliano haya mazuri yenye manufaa kwa ustawi wa halmashauri” ameongeza Dc Muro
Miezi mitatu iliyopita Dc Muro alikutana na wawekezaji hawa na kuwashawishi kuwekeza ikungi na leo tumefanikiwa kupata rasmi uwekezaji huu mkubwa, nataka kuwahakikishia wananchi leo tumeongeza thamani ya kilichopo Ikungi
Dc Muro amemshukuru Mheshimiwa, Rais. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza vizuri diplomasia ya uchumi na sasa matunda yameanza kuonekana katika wilaya ya Ikungi
Imetolewa na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ikungi