Na Abby Nkungu, Singida
MKOA wa Singida umefanikiwa kuongeza kiwango
cha uandikishaji wanafunzi elimu ya awali kwa zaidi ya asilimia tisa
kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha sekta hiyo
kuanzia ngazi ya chini katika kumwezesha kila mtoto kupata haki ya msingi ya
elimu.
Mkuu wa mkoa, Dk Binilith Mahenge alibainisha
hayo mjini hapa katika taarifa yake juu ya Mafanikio mbalimbali ya mwaka mmoja
wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Mahenge alisema kuwa katika kipindi hicho,
kiwango cha uandikishaji wanafunzi wa darasa la Awali kimeongezeka kutoka
wanafunzi 43,801 sawa na asilimia 87 mwaka jana hadi 49,785 sawa na asilimia
96.6 ya lengo kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Alieleza kuwa pamoja na sababu nyingine,
kupanda kwa uandikishaji huo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na
kuanzishwa shule shikizi 77 kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huu katika
kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Naye Ofisa elimu mkoa wa Singida, Maria Lyimo
alifafanua kuwa shule hizo shikizi zina wanafunzi wa chekechea takriban 8,700
ambao wanaendelea na masomo kama kawaida.
“Wewe unajua Singida ni
miongoni mwa mikoa inayotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa
ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-
MMMAM). Kwetu sisi, hii ni sehemu ya utekelezaji wa Programu hiyo
ambayo uzinduzi wake ulifanyika Dodoma mwaka jana” alisema Ofisa elimu huyo.
Mmoja wa walimu katika shule shikizi Mwembe
Mmoja nje kidogo ya mji huu, Fatuma Yusufu alisema kuwa shule hizo zimesaidia
kupunguza utoro, kuongeza usikivu darasani na kuwafanya watoto kupenda elimu.
“Wapo watoto katika baadhi ya shule
wanatoka mbali na wanatembea zaidi ya kilomita 14 kwenda shule na
kurudi nyumbani. Hebu fikiria, mtoto wa chini ya miaka minane anayesoma chekekechea
anafika shuleni kachoka, anapiga miayo tu kwa njaa na uchovu kisha
anachapa usingizi darasani hivyo hasomi chochote” alieleza Mwalimu huyo.
Nao baadhi ya wazazi na walezi wamemshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizosaidia katika ujenzi wa shule
hizo shikizi ili kuondoa adha; hasa kwa watoto wanaosoma Chekechea.
“Watu wamekuwa wakijiuliza kwa nini wazazi
wengi wanapenda kupeleka watoto wao wadogo shule binafsi za Awali.
Sababu ni kama hiyo…..mazingira ya shule zetu nyingi za Serikali
hayakuwa rafiki kwa watoto wadogo. Kwa kweli Mama ameupiga mwingi kwenye elimu,
sekta hii itapanda sana” alisema Ntandu Mumwi, mkazi wa Utemini.
Rehema Ali mkazi wa Mandewa pamoja na
kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za madarasa hayo, alisema bado
kuna haja ya kuboreshwa zaidi mazingira; hasa kwa watoto wadogo ambao hupenda
michezo mbalimbali jambo ambalo pia linaungwa mkono na Wataalam wa masuala ya
watoto.
Tanzania ni Nchi ya kwanza katika ukanda wa
Afrika Mashariki kuifanya elimu ya Awali kuwa ya lazima kwenye Sera ya elimu na
mafunzo ya mwaka 2014 ili kuijumuisha elimu ya Awali katika elimu ya msingi kwa
kuzitaka shule zote za msingi kuwa na darasa la Awali kwa watoto walio chini ya
miaka mitano.