Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Michezo wa Mwaka 2021 – 2031 baada ya kufungua Kikao Kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Tanzania Bara kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Saint Gaspar jijini Dodoma, Aprili 5, 2022. Kushoto ni Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha nakala za kitabu cha Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Michezo wa Mwaka 2021 – 2031 baada ya kuuzindua kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Saint Gaspar jijini Dodoma, Aprili 5, 2022. Wa pili kushoto ni Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, kulia ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul na kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Kikao Kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Tanzania Bara wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua kikao hicho kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Saint Gaspar jijini Dodoma, Aprii 5, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Saint Gaspar jijini Dodoma kufungua Kikao Kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Tanzania Bara , Aprili 5, 2022. Kulia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
- Awahimiza Watanzania kufanya mazoezi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini imekuwa kwa kiasi kikubwa na imeanza kuleta tija kwa maisha ya Watanzania kutokana na miongozo thabiti inayotolewa na Serikali
“Kwenye Sanaa tumeona namna ambavyo nchi hii imeweza kutangazwa vizuri na wasanii wengi kutoka ndani ya nchi, haya yote ni matokeo ya uratibu unaofanywa na Wizara, kwenye michezo tumeona namna ambavyo leo hii Tanzania inavyopata heshima kwa kuwa na timu za michezo mbalimbali zikifanya vizuri ndani na nje ya nchi.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 5, 2022) wakati akifungua kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo wa Mikoa na Halmashauri kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma.
Amesema Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeonesha kuwa na uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wengi na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla huku akitanabaisha kuwa sasa kwenye michezo kuna vijana wa Kitanzania wanaocheza michezo ya kulipwa katika nchi mbalimbali.
“Nitumie fursa hii kuwaasa Watanzania kuwa na moyo wa kuthamini kazi za wasanii wetu, Sanaa inatangaza taifa letu na utamaduni wetu pia unaitangaza nchi yetu.”
Waziri Mkuu amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili kuwawezesha Maafisa Utamaduni na Michezo kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Ni Muhimu sasa TAMISEMI kuhakikisha mnatambua umuhimu wa kitengo cha Michezo, Sanaa na Utamaduni katika Halmashauri kuwa ni moja kati ya vitengo muhimu ndani ya Halmashauri, na pia wapate nafasi ya kutumia taaluma yao kutekeleza majukumu ndani ya Halmashauri ili tuone mafanikio ya sekta hii”.
Aidha Waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha inaandaa vikao kazi vya maafisa utamaduni mara kwa mara ili kuwawezesha kupata mafunzo, kujua changamoto wanazopitia katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kupata muda wa kufanya tathmini ya maazimio yanayotolewa katika vikao kazi hivyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara hiyo kuhakikisha inaboresha uratibu na usimamizi wa mafunzo ya wataalamu wa michezo Nchini ili kuongeza idadi ya wataalam hao hususan katika mpira wa miguu kwani kumekuwa na kiwango kikubwa cha wakufunzi wa mpira kutoka nje ya nchi huku Tanzania ikikosa wakufunzi wanaofundisha nje ya Tanzania.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Maafisa Utamaduni Sanaa na Michezo kusimamia na kuratibu vikundi mbalimbali vya mazoezi vilivyo katika maeneo yao. “Ni jukumu lenu kuhakikisha kila Afisa katika eneo lake anahamasisha na kuanzisha vikundi vidogo vidogo vya mazoezi ili kuwe na hamasa ya michezo kwa watu wa rika zote pamoja na kuibua na kukuza vipaji kwa vijana mbalimbali kwa kuratibu shughuli za makundi ya wasanii.”
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Omari Mchengerwa amesema Sekta ya michezo nchini imeendelea kuimarika na imechangia zaidi ya shilingi Bilioni 1.7 katika pato la Taifa na Wizara imeendelea kujipanga ili kuhakikisha mchango wa Sekta hiyo unafikisha shilingi Bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Wizara imeendelea na mikakati ya kufanya maboresho ya miundombinu ya michezo, na hapa ni pamoja na maboresho ya ujenzi wa viwanja vya michezo katika shule 56 ambapo kila Mkoa utakuwa an Shule mbili za michezo, ikienda sambamba na uanzishwaji wa mkakati wa kuibua vipaji wa mtaa kwa mtaa.”
Katika kikao hicho Waziri Mkuu amezindua Mkakati wa Maboresho ya Sekta ya Michezo wa Mwaka 2021/2031 ambao utatoa muongozo wa kusimamia na kuboresha sekta ya michezo Nchini.