Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ametoa rai, kwa madiwani kuhakikisha wanaleta matokeo chanya katika kutatua kero za wananchi .
Amewaasa kusimamia majukumu yao na kujipanga kupata ufumbuzi kwa vipaombele vya maeneo Yao husika.
Akifunga mafunzo ya siku mbili ambayo yameandaliwa na Mbunge viti maalum Pwani ,Hawa Mchafu na kufadhiliwa na kituo Cha haki za binadamu , Kunenge alisema viongozi hao wamepewa dhamana ,na dhamana hiyo itawahukumu baadae endapo hawatawatumikia wananchi.
“Tukuchukue nafasi zetu ,ziwe katika nafasi za kiuchumi, ili kujiletea maendeleo,Rais wetu Samia Suluhu Hassan hapumziki ,kila siku anafanya jipya ,na sisi watendaji wake tunapaswa kufanya Yale ambayo yataacha alama wakati tukiwa hatupo madarakani”
Kunenge aliwaomba pia madiwani hao kupigania haki za watoto ,kukemea mimba za utotoni na Mila na desturi ambazo Ni kandamizi ili kupunguza matukio ya aina hiyo ndani ya jamii.
Awali mbunge viti maalum Pwani, Hawa Mchafu alisema kutokana na matukio ya Mila na desturi zisizo rafiki kwa watoto wa kike,utoro mashuleni na mimba na ndoa za utotoni katika mkoa huo ndicho kilichomsukuma kutafuta ufadhili ili madiwani wapate mafunzo mbalimbali ikiwemo kupata ujasiri wa kupambania kesi za matukio ya aina hii.
Alisema ,amealika madiwani wote 56 wanawake kwa mkoa huo ambao wamejitokeza Ni 54 ambapo Ni sawa na asilimia 96.4.
” Nampongeza Kunenge ,nampongeza na kumshukuru Rais Samia kwa Kuwa wanamaendeleo wa kwanza Mkoani Pwani, Namshukuru Rais kwa kuhakikisha Tisa za bweni zinazotakiwa kujengwa nchini mojawapo itajengwa Mkoani hapa “
” Ujenzi wa shule hizi utakwenda kupunguza mimba za utotoni ,watoto wanapaswa wasome katika Mazingira bora na ya kuwalinda ili kuhakikisha wanasonga kupata taaluma Yao “alisema Mchafu.
Vilevile Mchafu ,aliwashauri madiwani wanawake kujifunza kuwekeza kabla ya kukoma nafasi zao za Uongozi ilihali wawe na pa kuanzia.
Nae ofisa wa Jinsia (wanawake, watoto na wenye ulemavu kutoka kituo cha haki za binadamu ,Gutruda Dyabene alieleza wametoa mafunzo ya siku mbili ili kujadili changamoto za Uongozi wanazopata madiwani wanawake pamoja na nanma gani wanaweza kuthubutu kugombea nafasi mbalimbali kama ilivyo kwa wanaume.
Alisema baada ya mafunzo,wataandaa mipango kazi katika Halmashauri zao kufanyia kazi eneo la wanawake, mimba za utotoni,na utoro.
Diwani viti maalum Mjini Kibaha ,Selina Wilson alisema mafunzo hayo yatakwenda kuwasaidia katika majukumu yao .
Aliomba mkuu wa mkoa wa Pwani , kuzungumza na vyombo vya ulinzi na Usalama maana baadhi ya wananchi wanakwama maeneo hayo Mara wanapotaka Sheria itende haki katika kesi za mimba za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia.
Alimshukuru Mbunge Hawa Mchafu kwa kuwajengea uwezo kwani mafunzo hayana mwisho.