Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Lupembe,Joram Hongoli (kushoto) wakipitia orodha ya vijiji vilivyopata na visivyopata katika jimbo hilo ili vile ambavyo bado viweze kupatiwa umeme
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wanakijiji wa Lole kabla ya kuwasha umeme katika kijiji hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, mkoani Njombe.
Baadhi wa wanakijiji wa Lole, katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, mkoani Njombe, wakimshuhudia, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( haonekani pichani) akiwasha umeme katika moja ya nyumba za ibada katika kijiji hicho.
Wanakijiji wa Kijiji cha Ninga, katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, mkoani Njombe,wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kuhusu mradi wa usambazaji wa umeme vijiji (REA), kabla ya kuwasha umeme katika kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( kulia) akitoa maelekezo ya kuboresha na kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijiji ( REA) kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo wa Kampuni ya JV Mufindi Power Service Ltd na Hegy Engineering Service Ltd, Shirika na Umeme nchini (Tanesco), na Wakala wa Nishati vijijini REA.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, (kushoto) akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Ninga, huku watoto nao wakimsikiliza kwa shauku ya kupata umeme.
Baadhi ya wanakijiji wa Ninga, wakipiga pushapu kwa furaha ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli ya kuwapatia wananchi maendeleo ikiwemo nishati ya umeme.
……………………..
Na Zuena Msuya , Njombe
Waziri Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amewagiza wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Usambazaji umeme Vijijini, kuweka miundombinu ya umeme katika maeneo yaliyoidhinishwa na Serikali za Vijiji kujengwa taasisi za umma kama vile shule, nyumba za ibada, vituo vya afya pamoja na masoko , hata kabla ya ujenzi kuanza.
Dkt. Kalemani alisema kwa kufanya hivyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma ya umeme katika taasisi hizo pindi ujenzi wa majengo utakapokamilika hata baada ya mradi wa usambazaji umeme vijijini kukamilika.
Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo, Septemba 1,2019, wakati akiwasha umeme katika Kijiji cha Lole na Ninga pamoja na kukagua maendeleo ya mradi wa usambazaji umeme vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
“Wakandarasi wote nchini mnaotekeleza Mradi wa REA, hakikisheni maeneo yaliyoidhinishwa na serikali kujengwa taasisi za umma yanawekewa miundombinu ya umeme,hatutaki kuona taasisi zinajengwa lakini hakuna umeme wakati tayari mradi wa umeme ulikwishapita katika kijiji husika, hii itaendeleza azma ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma bora zaidi”, alisema Dkt. Kalemani.
Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA, awamu ya Tatu Mzunguko wa kwanza katika Mkoa wa Njombe ni Kampuni ya JV Mufindi Power Service Ltd na Hegy Engineering Service Ltd,
Kalemani aliweka wazi kuwa kumekuwa na changamoto kwa taasisi nyingi za umma,Vituo vya Afya pamoja na nyumba za ibada kukosa umeme na maeneo mengine miundombinu ya umeme kupita mbali zaidi, hivyo wahusika kushindwa kuunganishwa na huduma hiyo licha ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini kutekeleza katika maeneo hayo.
Vilevile alisema baada ya changamoto hiyo kutokea, wamebaini kuwa taasisi nyingi zilizokosa umeme ni zile zilizokuwa bado hazijajengwa ama ujenzi wake ulikuwa haujakamilika, kipindi ambacho wa mradi wa usambazaji umeme vijijini unatekelezwa.
Waziri wa Nishati. Dkt.Kalemani alieleza kuwa, maeneo yote yatakayoidhinishwa na serikali kujengwa taasisi za umma, vituo vya afya na nyumba za ibada lazima yawekewe miundombonu ya umeme wakati wa utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijiji unaoendelea sasa.
Aidha ameendelea kuwakumbusha wananchi wote nchini hasa waliopo vijijini kuendelea kulipia shilingi 27,000 ikiwa ni gharama ya kuunganishiwa umeme pia kutandaza nyaya katika nyumba zao kurahisisha zoezi la kuwaunganishia umeme utakapowafikia.
Aliendelea kusisitiza kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha mradi huo unawafikia na kuwanufaisha wananchi wote hasa wale walio vijijini kwa gharama nafuu, hivyo haitakuwa busara endapo walengwa wa mradi huo watashindwa kuchangamkia fursa hiyo.
Waziri Kalemani, alisesema hadi kufikia Januari, 2020,tayari vijiji vyote vilivyokuwa katika mpango wa kupata umeme wa mradi wa REA awamu ya tatu Mzunguko wa kwanza vitakuwa tayari vimeunganishiwa umeme nchini kote na kuendelea na REA mzunguko wa tatu awamu ya pili ambao ukomo wake ni Juni, 2020.