Wadau wa sekta binafsi na umma wakiwa ukumbini kwenye kikao cha kutoa maoni ya rasmu ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022
…………………………………………………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara imewakututanisha wadau wa Sekta binafsi na umma kwa lengo la kutoa maoni ya rasmu ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2022.
Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Gold crest uliopo Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mkurugenzi msaidizi wa Uwekezaji Neema Maregeli, amesema lengo la mkutano huo ni kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha rasmu ya sera ya Taifa.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikitunga sera na sheria mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya Uwekezaji na biashara hapa Nchini.
“Mwaka 2021 Wizara ilifanya tathimini ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 ambayo inamalengo mahususi sita, na malengo nane ya kisekta ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wa ndani wakukuza Uwekezaji,kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa kwaajili ya mauzo ya nje,kuvutia Uwekezaji kutoka nje ya Nchi,kuhimiza na kuvutia matumizi ya Teknolojia za kisasa katika Uwekezaji,kuweka mfumo mzuri na wawazi wa kisheria na kuondoa urasmu katika taratibu za upatikanaji wa vibali vya uwekezaji”,amesema Maregeli.
Aidha, amesema kuwa sera hiyo inatoa muongozo wa Uwekezaji katika Sekta mbalimbali za uchumi zikiwemo sekta za viwanda, utalii,usafirishaji,kilimo na madini.
Kwaupande wake Meneja wa kituo cha Uwekezaji kanda ya ziwa Girson Ntimba, ambae ni mshiriki wa mkutano huo amesema kuwa sera hiyo itawezesha kufanikisha Uwekezaji Nchini na itaongeza kasi katika kuchochea maendeleo ya uzalishaji na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Amesema kwa upande wa Kanda ya ziwa wamejipanga kuhamasisha wawekezaji wa ndani kuongeza mitaji ili waweze kutoa ajira kwa vijana hali itakayosaidia kuondokana na umasikini.
Nae Afisa sera kutoka Taasisi ya sekta binafsi Tanzania(TPSF), Faith Gugu amesema jukumu la sekta binafsi ni kushirikiana na Serikali kwa ukaribu ili kuweza kuhakikisha Tanzania Kuna sera,sheria na taratibu mbalimbali ambazo ni wezeshi kwa mfanyabiashara na muwekezaji.