Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Shirika lisilo la kiserikali
la Investing in Children and Strengtherning their Societies (ICS ) linalohusika
na masuala mbalimbali ikiwemo malezi na makuzi bora ya watoto,ulinzi na usalama
kwa watoto na wanawake limetoa mafunzo kwa wafanyakazi wake 22 kuwajengea uwezo
kuhusu mkakati wa namna ya kutoa elimu ya malezi na makuzi bora ya watoto kwa
njia ya kidigitali (Digital Parenting) kupitia Programu Tumishi (Aplikesheni)
ya Parent App.
Akizungumza wakati wa mafunzo
hayo ya siku nne yaliyoanza leo Jumatatu Machi 28,2022 katika ukumbi wa
Vigimark Hotel Mjini Shinyanga, Mkurugenzi wa Shirika la ICS Kudely
Sokoine amesema timu ya ICS inajifunza na
kujinoa kila siku kuendana na kasi ya kukua kwa teknolojia duniani.
Amesema mafunzo hayo
yanafanyika kwa njia ya mtandao (Tele conference) na shirika la Crown Without
Borders South Africa na wafanyakazi wa ICS Tanzania wapatao 22 wanajengewa
uwezo kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi mpya wa Parenting for Life Long
Health (PLH).
“Mafunzo kwa wafanyakazi 22
wa Shirika la ICS kwa ajili ya kujifunza mkakati wa namna ya kutoa elimu ya
malezi na makuzi bora ya watoto kwa njia ya kidigitali (Digital Parenting) kupitia
Parent App ni sehemu ya kujijengea uwezo
kabla ya kuanza utekelezaji yanafanyika kwa njia ya mtandao (Tele conference)
na shirika la Crown Without Borders South Africa. Baada ya mafunzo haya kazi ya
utekelezaji itaanza katika mkoa wa Mwanza na Shinyanga ”,amesema Kudely.
“Mafunzo haya ni sehemu ya
utekelezaji wa mkakati wa kidunia wa kufikisha elimu ya malezi na makuzi bora
ya mtoto ili kuondoa ukatili dhidi ya
watoto na wanawake (The Global Parenting Initiative) . Sisi ICS tumeanza mafunzo
haya ili kutekeleza mkakati huu kupitia mradi wa Parenting For Life Long Health
(PLH) ambapo tunashirikiana na taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR),
Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza na Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika
Kusini”,ameeleza Kudely.
Amefafanua kuwa Shirika la
ICS litakuwa linafanya utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na taasisi ya
Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza na Chuo
Kikuu cha Cape Town Afrika Kusini na kufanya utafiti wa kina ili kutambua ni
kwa kiasi gani kufikisha elimu ya malezi na makuzi bora ya mtoto kwa njia ya
kidigitali na inaleta tija ili kupunguza ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
“Tunaanza utekelezaji wa mradi huu mkoani Shinyanga na Mwanza na awamu
ya kwanza tumepanga kufikia wazazi/walezi 1100 na awamu ya pili tunatarajia
kutanua utekekezaji na kufikia mikoa Zaidi ya 6 Tanzania na kufikia wazazi
/walezi wasiopungua 6000”,amesema Kudely.
Ameongeza kuwa Utekelezaji wa
mpango huu umekuja kama sehemu ya ubunifu (Innovation) wa namna ya kufikisha
elimu katika jamii kwa njia ya teknolojia na kuwafikia wanufaika wengi zaidi
ili kuleta mabadiliko na kuchangia kuondoa ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
“Na sisi kama ICS kila
wakati tunapotekeleza afua zetu tunajifunza na kuja na ubunifu ambao unaweza
kuleta tija Zaidi katika jamii lakini pia kufanya tafiti zitakozopima na
kuthibitisha afua tunazotekeleza zinaleta matokeo chanya (Evidence Based
Intervention)”,amesema
“Sisi kama ICS na washirika
wetu (Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Chuo Kikuu cha Oxford
Uingereza na Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika Kusini) tunajitahidi kila siku
kuwa wabunifu na kuja na mikakati ambayo inaweza kutumia rasilimali kidogo na
kuleta matokeo makubwa katika afua zetu zote tunazozitekeleza”,ameeleza.
Amefafanua kuwa Utekelezaji wa mradi huu
(Pareting for Life Long Health-PLH) wa kutoa elimu ya malezi na makuzi ya bora
ya mtoto kwa njia ya kijitali utachangia mpango wa dunia (The Global Parenting
Initiative-GPI) wa kufikisha elimu ya malezi wa wazazi/malezi na pia mpango wa
Taifa (NPA-VAWC) wa kupunguza Ukatili dhidi ya watoto wa wanawake na watoto.
“Wazazi/Walezi wengi wana
simu kwa hiyo tumebuni namna ya kuwafikishia elimu kwa njia rahisi kabisa na
inayotumia muda mfupi maana ParentApp
mzazi/mlezi anaweza kuitumia hata wakati hayupo kwenyeInternet akajifunza na
kupata ujumbe murua kabisa kuhusu malezi na makuzi bora ya watoto”,amesema
Kudely.