Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo akikabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo kwa mmoja wa washiriki
Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo akiwahutubia washiriki wa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa TANePS yaliyofanyika jijini Arusha
Baadhi ya washiriki wakiwa katika mafunzo kwa vitendo kuhusu matumizi ya mfumo wa TANePS .
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imetoa wito kwa Taasisi nunuzi kuwaruhusu watumishi wa vitengo vya usimamizi wa manunuzi pamoja na mifumo ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kushiriki kwenye mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa njia ya Mtandao ili ziweze kuunganishwa na kufanya manunuzi yake kwa kutumia mfumo huo.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku sita kuhusu matumizi ya Mfumo huo unaojulikana kwa jina TANePS (Tanzania National e-Procurement System) kwa maafisa 110 wa vitengo vya usimamizi wa manunuzi na Tehama kutoka Taasisi 44.
Mhandisi Kapongo amezisisitiza Taasisi nunuzi kuhakikisha zinaunganishwa na kisha kufanya manunuzi yake kwa kutumia mfumo huo wa TANePS ili kukidhi matakwa ya sheria ya manunuzi ya umma pamoja na uamuzi wa Serikali kutaka taasisi zote za umma kuunganishwa na TANePS ili ziweze kufanya manunuzi yote kupitia mfumo huo kwa lengo la kurahisisha michakato ya manunuzi kufanyika kwa ufanisi na tija zaidi na kuhakikisha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha.
Amezitaja baadhi ya faida za mfumo wa TANePS unaosimamiwa na PPRA kuwa ni kupunguza gharama na muda kwenye michakato ya manunuzi serikalini pamoja na kuongeza uwazi, ushindani na usawa kwa wazabuni na watoa huduma wanaoshindania zabuni mbalimbali zinazotangazwa na Taasisi za Umma.
“TANePS inawezesha mchakato wote wa manunuzi serikalini kufanyika kielektroniki ambapo hakutakuwa na sababu ya wazabuni kutumia muda mwingi kutembelea ofisi za Taasisi za Umma pale wanapotaka kushindania zabuni, pia hawawezi kukutana ana kwa ana na watumishi wa taasisi za umma kwa kuwa kila kitu kinafanyika mtandaoni,”alisema Mhandisi Kapongo.
Aidha, Mhandisi Kapongo ametoa wito kwa wafanyabiashara, wazabuni na watoa huduma kuhakikisha wanajisajili kwenye mfumo huo ili waweze kushiriki au kushindania zabuni mbalimbali zinazotangazwa na taasisi za umma.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2019, wataalamu kutoka PPRA wamepiga kambi jijini Arusha kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya TANePS kwa awamu tofauti, programu inayotarajiwa kuwa endelevu ili kutoa fursa kwa wataalamu wa manunuzi kwenye taasisi zote za umma kupata fursa ya mafunzo hayo. Tangu kuanza kwa programu hii kabambe jumla ya watumishi 204 kutoka taasisi za umma 75 wameshapatiwa mafunzo hayo, ambapo wahusika wanapaswa kutembelea tovuti ya mfumo (www.taneps.go.tz) au tovuti ya PPRA (www.ppra.go.tz) ili kupata zaidi maelezo ya namna kujisajili kushiriki.
Mafunzo haya yanagharamiwa na Serikali pamoja na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).