********************
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amebainisha kuwa Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha inaanzisha vijiji vya kilimo vya vijana katika maeneo ya kilimo nchini kupitia mfumo wa mashamba makubwa ya pamoja “block farms” ili kuchochea ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo jana tarehe 27 Machi, 2022 Jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi kwenye Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake na Vijana yaliyoandaliwa na Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake na Vijana Tanzania (TABWA) na katika uzinduzi wa mpango wa kushirikisha Vijana na wakina mama kwenye mnyororo wa kuongeza thamani wa mazao ya kilimo
“Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Toboa na Kilimo, tumedhamiria kuanzisha mfumo wa mashamba ya pamoja ya vijana (block farming), ili vijana walime, wajenge makazi yao na waishi hapo hapo, hii itakuwa ni ya hatua kubwa ya mfumo mzuri wa kuwawezesha vijana kwenye utatuzi wa chamgamoto ya Ajira na itavutia vijana wengi kuingia kwenye kilimo.
Kupitia program hii Vijana wataandaliwa ardhi ambayo itakuwa imepimwa Afya ya udongo,itakayowekwa mifumo ya umwagiliaji,upatikanaji wa pembejeo na baadaye kutafutiwa masoko ya mazao watakayozalisha.
Tunamshukuru Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kupitia benki kuu ya Tanzania juu ya riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo,ambapo hivi sasa riba ya mikopo ya kilimo imeshuka mpaka chini ya 10% kwa Taasisi nyingi za fedha na hivyo kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wadau wa kilimo” Alisema Mavunde
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde alipokea taarifa ya Vijana waliokwenda kwa ufadhili wa serikali katika maonesho ya Biashara ya Dubai Expo na maonesho ya Kilimo Mjini Konya,Uturuki na kuwataka kutumia ujuzi na fursa walizopata kwa ajili ya kuendeleza kilimo nchini Tanzania na kuwa mabalozi wazuri wa ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo.
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa TABWA, Bi. Noreen Mawala amesema kuwa Taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanawake na vijana wengi zaidi wanachangamkia fursa nyingi zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo na kuishukuru serikali kupitia wizara ya kilimo kwa hamasa kubwa wanayoitoa katika kuhakikisha ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo ili kutatua changamoto ya Ajira miongoni kwa Vijana na kupunguza umaskini wa wananchi.