Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima , Akizungumza wakati wa Hafla ya Somo na Mwari iliyofanyika kwenye Ukumbi City Garden, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya BREMBO, Asnat Hamis, akiongea wakati wa hafla ya Somo na Mwari iliyofanyoka jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja ya Waziri Dkt. Dorothy Gwajima, akiwa na Waandaaji wa Hafla ya Somo na Mwari, ilifanyika kwenye Ukumbi wa City Garden jijini Dar es Salaam.
Mme wa Mkurugenzi wa BREMBO Bw. Hamis, akikabidhi Tuzo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima wakati wa Hafla ya Somo na Mwari iliyofanyika jijini DSM
Baadhi ya Washiriki wa Hafla ya Somo na Mwari inayofanyika katika Ukumbi wa City Garden, Wakimsikiza Waziri Gwajima (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo.
Picha na Habari Vyote na WMJJWM
********************
Na MJJWM- Dar Es Salaam.
Serikali imelitaka kundi la wanawake kuwa mstari wa mbele kuongoza jamii kujitokeza kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, ambapo kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za watu wake na kuisaidia kupanga mipango mizuri kwa kuihudumia jamii.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye alikuwa mgeni rasmi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwenye hafla ya Somo na Mwari iliyoandaliwa na taasisi ya Brembo inayo milikiwa na Asnat Hamis iliyofanyika Machi 26, 2022 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuwatambua na kuwatengenezea mazingira wezeshi wanawake ambao wameonesha jitihada za kumkomboa mwanamke wa jamii ya kitanzania.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuona kuna kuwa na usawa wa kijinsia ndani ya Jamii, hivyo wakina mama mnaojitokeza kama akina Asnat mzidi kujitokeza, ili muweze kutambulika kitaifa na kimataifa, tunapokwenda kwenye majukwaa ya kimataifa, tukiulizwa wanawake wa taifa lako wako wangapi tuwe na cha kusema, lakini zaidi sana tuseme tukiwa na takwimu sahihi, hivyo kujitokeza kwenye Sensa na kuhesabiwa ni muhimu sana” alisema Mhe. Waziri Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema wanawake Tanzania ni takribani asilimia 51.04 huku takwimu za kimataifa zikionesha kuwa wanawake ni nusu ya watu wote duniani na wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi ambapo kitaifa asilimia themanini (80%) ya nguvu kazi ya Sekta ya kilimo ni wanawake na huzalisha asilimia sitini (60%) ya chakula chote hapa nchini.
Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua kadhaa za kuboresha kipato na kuondoa umaskini kwa wanawake wa Tanzania zikiwemo kutenga jumla ya Shilingi bilioni 62.68 katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwenye halmashauri zote nchini.
Aidha, amesema hadi kufikia Juni 30, 2021 jumla ya Shilingi bilioni 53.81 zilikopeshwa kwa vikundi 7,993 vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu sawa na 86%, ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bil. 28.17 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake 4,894 vilivyozalisha ajira 52,428, nchini.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa kupitia Benki ya Biashara kwenye dirisha la mikopo, jumla mikopo yenye thamani ya shilingi Bil. 22.3 imetolewa kwa wanawake wajasiriamali wapatao 6,326 kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi April, 2021 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa, Serikali imewezesha kutungwa kwa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Namba 5 (1999), Kifungu cha 20(1), ambacho kinatoa nafasi kwa wanawake kumiliki Ardhi. Hatua hiyo imeleta matokeo ya ongezeko la umiliki wa ardhi kwa wanawake kutoka asilimia 9 (2014) hadi asilimia 25 Mwaka 2017.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Brembo Bibi Asnat Hamis amesema Taasisi yake imejikita kuelimisha wanawake juu ya mfumo wa uzazi kutokana na wanawake wengi kuweka vitu kwenye via vya uzazi ambavyo mwisho huwasababishia madhara ya afya.
“Taasisi imeweza kuwakomboa wanawake wengi na madhila kutokana na kutoa elimu lakini pia tumefanikiwa kuwafikia wanawake zaidi ya 2500 ambao pamoja na kuwapatia elimu lakini pia tumewapatia mitaji kupitia majukwaa ya ushirikiano na mshikamano” alisema Asnat.