Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira yaiagiza Wizara na Taasisi zake kuendelea kuongeza kasi na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira imeiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi zake kuendelea kuongeza kasi na ubunifu katika utekelezaji wa jitahada mbalimbali za kuendeleza sekta hiyo ili kukuza uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) wakati Wizara hiyo ilipowasilishaTaarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2021/2022 ya Wizara na Taasisi zake kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, Machi 23, 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi na utekelezaji wa jitihada na mikakati mbalimbali ya kuendeleza Sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara ili kuongeza uwekezaji, kukuza biashara na uchumi shindani wa viwanda.
Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) aliihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ili kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.
Awali, akitoa Taarifa ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo pamoja na bajeti ya Wizara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara alieleza kuwa Wizara imetekeleza majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha 2021/22 ambayo yameleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Prof. Kahyarara alielezea utekelezaji wa majukumu hayo ikiwemo uhuishaji wa Sera Sheria na Mikakati inayohusu uendelezaji wa sekta hiyo, uhamasishaji wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, uendelezaji wa kongani za viwanda katika maeneo mbalimbali nchini, uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara, usimamizi wa viwanda vidogo na biashara ndogo, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uendelezaji wa mahusiano na majadiliano ya kibiashara baina ya nchi, kikanda na kimataifa.
Aidha, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo zilipata fursa ya kuwasilisha utekelezaji wa bajeti ya taasisi zao kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Taasisi hizo ni pamoja na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA), Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Taasisi nyingine zilizowasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti zao kwa Wajumbe wa Kamati hiyo ni Pamoja Baraza la Ushindani (FCT), Wakala wa Vipimo (WMA ) Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo na Biashara ndogo (SIDO), Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia vijijini ( CAMARTEC) na Shirika la Uhamdisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO).