Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Samas kushoto,akimsikiliza meneja waRuwasa wilayni Masasi Juma Yahaya kuhusu ujenzi wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa wilayani humo.
Tenki la kuhifadhia maji linalojengwa katika kijiji cha Chakama ambapo mara litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 za maji na litahudumia takribani wakazi 3,500
Ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Mwindi kata ya Mbawala linalojengwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Mtwara,tenki hilo ni sehemu ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingi milioni 804,597,262.90 ambao utahudumia wananchi wa kata ya Mbawala wilayani Mtwara.
Kaimu Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Ruwasa wilaya ya Mtwara Mhandisi Aloyce Milyangula kulia na Afisa maendeleo ya jamii Clever Paul wakikagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi atakayehudumia mradi wa maji wa Mwindi kata ya Mbawala utakaotoa huduma ya maji katika vijiji vya kata hiyo.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Mhandisi Aloyce Milyangula akikagua nyumba ya kuhifadhi mashine ya kusukuma maji kwenye mradi wa maji Mwindi unaotekelezwa na Ruwasa kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vinavyounda kata ya Mbawala wilayani Mtwara.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani Mtwara Mhandisi Aloyce Milyangula kulia na Afisa maendeleo ya jamii Clever Paul kushoto na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mwindi kata ya Mbawala Suzana Chinguku katikati, wakiangalia kisima kinachotarajiwa kuhudumia wakazi wa kata ya Mbawala wilayani humo mara ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa na wizara ya maji kupitia Ruwasa katika kijiji cha Mwindi utakapokamilika.
Sehemu ya mabomba ya maji yakiwa tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaojengwa katika kijiji cha Mwindi kata ya Mbawala wilayani Mtwara ambao mara utakapokamilika unatajwa kumaliza kabisa changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Mbawala.
……………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Mtwara
TATIZO la ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Mbawala wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, limepatiwa ufumbuzi baada ya Wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)wilayani humo kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji.
Mradi huo utakagharimu jumla ya Sh. milioni 804,597.262.90 fedha zilizotolewa na Serikali kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uvico-19.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Mtwara Mhandisi Aloyece Milyangula alisema,mradi huo utawanufaisha wakazi wa vijiji vya Mwindi,Mbawala,Nang’awanga Nachuma,Misufini,Kilomba Nalunga,Migombani.
Milyangula alisema,ulianza kutekelezwa mwezi Januari na unatarajia kukamilika mwezi Mei mwaka huu ambapo wanufaika wa mradi huo ni wakazi 1,1598.
Alisema,mradi wa maji Mwindi unatekelezwa kwa kutumia mkandarasi na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kutoa fedha ambazo zitasaidia wananchi wa vijiji hivyo waondokane na kero kubwa ya maji safi na salama hasa ikizingatia kuwa wananchi wa maeneo hayo hawana chanzo mbadala.
Alisema,mradi utakapokamilika utawanufaisha na kubadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja na kuchochea uchumi wa wilaya,mkoa wa Mtwara na Taifa kwa jumla.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mwindi Issa Namwewe, ameshukuru kupata mradi huo wa maji kwani kwa muda mrefu kilio kikubwa cha wananchi wake ni ukosefu wa maji safi na salama.
Alisema,wananchi wa Mwindi hawakuwa na chanzo chochote za kupata maji, badala yake walilazimika kwenda kutafuta huduma hiyo kwenye vyanzo vya asili.
Kwa mujibu wake,vyanzo hivyo havikutosheleza mahitaji yao,jambo lililosababisha kero kubwa na wakati mwingine kutumia nguvu na hata kupigana ili kupata maji, ambayo hayakukidhi mahitaji ya familia zao.
Wakati huo huo, Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)wilaya ya Masasi imepokea jumla ya Sh.milioni 929,135,130.99 za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taif ana mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uvico-19.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji utakaowanufaisha wakazi 13,442 katika vijiji vinne vya Chidya,Chiwata,Msokosela na Chakama.
Meneja wa Ruwasa wilayani Masasi Juma Yahaya alisema, katika kijiji cha Chidya na Chiwata wananchi watakaonufaika na mradi huo ni 8,622 kijiji cha Chikama wananchi 2,426 na Msokosela ni 2,304.