Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, wakisaini mikataba mitatu ya msaada yenye thamani ya Euro Milioni 180 sawa na shilingi bilioni 469.4, kwa ajili ya kuboresha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba-Zanzibar, kuwa ya kijani na nadhifu, na Mradi wa Kidijitali wa Serikali Mtandao, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Mwanasheria kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Nyanzala Nkinga.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, wakiwaonesha wanahabari Hati za mikataba mitatu ya msaada yenye thamani ya Euro Milioni 180 sawa na shilingi bilioni 469.4, kwa ajili ya kuboresha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba-Zanzibar, kuwa ya kijani na nadhifu, na Mradi wa Kidijitali wa Serikali Mtandao, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, wakifurahi baada ya kusainiwa kwa mikataba mitatu ya msaada yenye thamani ya Euro Milioni 180 sawa na shilingi bilioni 469.4, kwa ajili ya kuboresha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba-Zanzibar, kuwa ya kijani na nadhifu, na Mradi wa Kidijitali wa Serikali Mtandao, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, wakibadilishana Hati za mikataba mitatu ya msaada yenye thamani ya Euro Milioni 180 sawa na shilingi bilioni 469.4, kwa ajili ya kuboresha masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba-Zanzibar, kuwa ya kijani na nadhifu, na Mradi wa Kidijitali wa Serikali Mtandao, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Dar es Salaam)
***********************
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 180 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 469 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu ikiwemo masuala ya kijinsia, kuboresha miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba, kuwa ya kijani na nadhifu, pamoja na kuendeleza Mradi wa Kidijitali wa Serikali Mtandao.
Mikataba ya Msaada huo imesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizaya ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Tanzania, na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mheshimiwa Manifredo Fanti, kwa niaba ya Umoja wa Ulaya.
Bw. Tutuba alisema kuwa kiwango hicho cha fedha ni sehemu ya ufadhili wa euro milioni 703 sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania trilioni 1.8 ambazo Umoja wa Ulaya umetenga kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo mitatu, ikiwa ni makubaliano ya ushirikiano wa miaka 7 kati ya Tanzania na Umoja huo, kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2027.
Alifafanua kuwa kati ya euro milioni 180 (469.4b) ambazo mikataba yake imesainiwa, kiasi cha euro milioni 70 (182 bilioni) kimetengwa kwa ajili ya mradi wa kuboresha masuala ya kijinsia ikiwemo kuimarisha uhuru, kuondoa ukatili wa aina zote katika maeneo ya umma na binafsi, shuleni, mahali pa kazi pamoja na mitandaoni kwa wanawake, wanaume, wasichana na wavulana.
“Mradi huu pia ambao utoaji wake wa fedha utapitia utekelezaji wa kibajeti, unahusisha kuwawezesha wanawake kiuchumi, ikijumuisha fursa endelevu za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kuimarisha usawa katika uongozi na maamuzi ikiwemo haki, amani na usalama” alisema Bw. Tutuba.
Bw. Tutuba alisema kuwa kiasi cha euro milioni 75 (195 bilioni) kimeelekezwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa ajili ya kuboresha mazingira ya miji ya Tanga, Mwanza na Kisiwa cha Pemba-Zanzibar, ili kuwezesha upatikanaji wa mapato ya ndani na maendeleo jumuishi ya uchumi katika maeneo ya mijini kwa makundi ya wanawake na vijana.
Alisema kuwa mradi wa kidijitali wa Serikali Mtandao umetengewa euro milioni 35 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 90 zitakazotumika kuboresha huduma za mitandao serikalini, kuongeza huduma za mitandao mijini na pembezoni mwa miji na kuendeleza sekta ya huduma za kifedha hapa nchini na kikanda.
Bw. Tutuba aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa na kuongeza kuwa uwekezaji wa Umoja huo hapa nchini tangu mwaka 1975, umefikia thamani ya euro bilioni 2.7 sawa na shilingi trilioni 6.6, ambapo kati ya fedha hizo, euro bilioni 2.4, sawa na shilingi trilioni 5.9 ni msaada na kiasi cha euro milioni 270.9 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 706.5 ni mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).
“Serikali inathamini msaada huu ambao umetumika kutekeleza miradi ya vipaumbele vya Serikali ikiwemo sekta ya miundombinu ya usafiri, viwanja vya ndege, nishati, kilimo, pamoja na miradi ya mazingira inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa Upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mheshimiwa Manifredo Fanti, alisema kuwa miradi iliyosainiwa itafungua fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana na kuboresha mazingira ya biashara kwenye maeneo yanayoguswa na miradi hiyo, pamoja na kuboresha haki kwa makundi mbalimbali.
Alisema kuwa kurejea kwa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya kufanya shughuli zake nchini kwa kushirikiana na Sekta ya Umma na Binafsi ni kielelezo cha ushirikiano imara uliopo kati ya pande hizo mbili na kwamba Umoja huo utaongeza ufadhili kwa Tanzania.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu akiwemo Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga.