Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida DC, Eliya Digha akizungumza wakati akitoa taarifa ya fedha walizozipokea kutekeleza miradi ya maendeleo. |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi akizungumza wakati akitoa taarifa ya fedha walizozipokea kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa akizungumza kwenye hafla hiyo. |
Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Singida
Alhajj Juma Killimbah amesema fedha za kutekeleza miradi zilizoletwa mkoani hapa
na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika
kipindi cha mwaka 2021/2022 kuanzia Julai 2021 hadi Februari 2022 ziwe chachu ya
maendeleo kwa wananchi na wanachama wa chama hicho.
Killimbah aliyasema hayo
katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanyika makao makuu ya chama hicho mkoani hapa
jana.
“Fedha hizi zilizotetwa na Mama yetu katika mkoa wetu ziwe
chachu ya maendeleo kwa mwaka huu unaokuja” alisema Killimbah huku
akishangiliwa na mamia ya Wananchi na Wana CCM waliohudhuria hafla hiyo.
Alisema miradi inayokuja mahala popote fedha hizo zinatafutwa na Rais wetu kwa
juhudi kubwa na wabunge wanasimamia
bajeti ili ije Singida kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Killimbah alitumia mkutano huo kumshukuru Rais Samia Suluhu
Hassan kwa mambo makubwa ya maendeleo
aliyoufanyia Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Lucy Boniphace akizungumza
kwenye hafla hiyo alisema kwa mwaka
mmoja alioongoza Rais Samia Suluhu Hassan Mkoa wa Singida umepiga hatua kubwa
ya kimaendeleo kwani wilaya zote wamepokea fedha nyingi za maendeleo.
Alisema sambamba na hilo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akikutana na makundi mbalimbali kwa lengo la
kuwasikiliza na kupokea maoni yao kwa ajili ya kujenga nchi yetu na kuwa huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa na kujiamini katika utendaji wake
wa kuongoza nchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida DC, Eliya Digha akizungumza wakati akitoa taarifa
ya maendeleo ya wilaya hiyo alimfananisha Rais Samia Suluhu Hassan na mwanamke
mmoja shujaa aliyetajwa kwenye Biblia aitwaye Esther ambaye alijulikana sana kwenye Taifa la
Waisrael.
“Rais wetu Mama Samia amefanya mambo mema na makubwa katika
nchi hii hivyo tunakila sababu ya kumpongeza” alisema Digha.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida Yohana Msita alisema Rais
Samia Suluhu Hassan hakika ameupiga mwingi hapa nchini kwa kazi kubwa
aliyoifanya ndani ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Alisema Rais Samia hakuna sehemu aliyoiacha bila ya kuifikia
kwa maendelea katika sekta zote na ameonesha uwezo mkubwa wa kuongoza nchi
ambapo aliwaomba watanzania kuendelea kumuombea kwa Mungu na kuunga mkono
jitihada zakezote za maendeleo anazozifanya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Mjini Lusia Mwiru
alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi
cha mwaka mmoja ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba Wana CCM wenye sifa ya
kugombea nafasi mbalimbali kujitokeza kuchukua fomu ya kugombea katika uchaguzi
wa ndani utaofanyika hivi karibuni.
Katika hafla hiyohiyo kila wilaya mkoani hapa ilitoa taarifa ya fedha
walizopokea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo walioifanya ambayo ziliwasilishwa
na Wenyeviti wa Halmashauri husika ambapo katika Wlaya ya Ikungi Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo Ally Mwanga alisema walipokea Sh.11,263,030,397 ambazo
zilitumika katika Elimu, Afya, Utawala, Mfuko wa Jimbo, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Singida (SUWASA).
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent
Msengi alisema wao walipokea Sh.10,960,988,976 kwa ajili ya kutekeleza miradi
hiyo huku Wilaya ya Itigi wakipokea Sh.7,435,318,522 na Manyoni Sh.10,505,419,366.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama walipokea
Sh.7,811,623,781, Singida DC
Sh.10,046,768,035, Singida Manispaa Sh.5,791,791,192, Sekretarieti ya
Mkoa Sh.875,552,414, Tanesco
Sh.63,507,622,522, Jumla Kuu ikiwa ni Sh.128,198,115,205.