*******************
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua mradi wa Lango la Naabi wenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 na ujenzi wa Serengeti Media Centre unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Korea (KOICA) wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5 katika Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mhe. Ally Juma Makoa (Mb) amesema miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa katika kuongeza idadi ya watalii nchini.
“Tunaishukuru sana Wizara kwa wazo zuri la kujenga Serengeti Media Center ambayo itasaidia kuitangaza nchi yetu Kitaifa na Kimataifa kwa sababu wageni watapata taarifa zote za hifadhi hii kupitia picha na matangazo” amefafanua Mhe. Makoa.
Akizungumzia mradi wa Lango la Naabi Mhe. Makoa amesema kuwa lango hilo litaleta taswira nzuri na litaongeza thamani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo mara tatu mfululizo imechukua tuzo mbalimbali.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema mradi wa Serengeti Media Centre umekamilika kwa asilimia mia moja na kwa upande wa mradi wa Lango la Naabi utakamilika kwa kadri fedha zinavyoendelea kuletwa.
Aidha, Mhe. Masanja amemuahidi Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kamati na kwamba Wizara itasimamia miradi hiyo vizuri.
Amesema lengo ni kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa nguvu zote ili kufikia malengo yaliyotarajiwa kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni kufikisha watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na pia kuongeza mapato yatokanayo na watalii kutoka Dola za Kimarekani bilioni 2.6 hadi Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.