******************
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara Prof. Godius Kahyarara ameitembelea kamati maalumu iliyoundwa ikishirikisha taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa huduma za pamoja kwa wawekezaji unaojulikana kama Tanzania Electronic Investment Window – TeIW.
Prof. Kahyarara amesema kuwa utengenezwaji wa mfumo huu ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alilolitoa akihitaji Wizara kuanzisha mfumo wa utoaji huduma kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwa na dirisha moja la huduma.
Prof. Kahyarara ameeleza kuwa timu hii imeanza kazi hii tangu tarehe 7 Desemba, 2021 ambapo walianza kutengeneza mfumo huu katika awamu ya kwanza na upo katika hatua ya mwisho kukamilika na kuanza majaribio na kwa awamu ya kwanza mfumo umeziweka pamoja taasisi saba ikiwemo NIDA, TRA, BRELA, ARDHI, KAZI, UHAMIAJI na TIC.
Amesema kuwa awamu ya pili ya utengenezwaji wa mfumo huu utahusisha taasisi tano zilizosalia ambazo ni TMDA, OSHA, TANESCO, TBS na NEMC
“Faida za mfumo huu ni kuwa utasaidia upatikanaji wa vibali vyote vinavyotolewa nchini kupatikana kwa urais na kwa haraka kwani huduma zote zitapatikana kupitia dirisha moja na mwekezaji ataweza kuomba vibali husika mahali popote alipo, pia utasaidia kufuatilia hatua za maombi ya uwekezaji”. Amesema Prof. Kahyarara.
Ameongeza kwa kusema kuwa kuanza kutumika kwa mfumo huu utasaidia kupunguza urasimu, gharama na muda kwani mwekezaji atapata huduma zote kupitia mfumo huu na sio kukutana na watoa huduma na hii itasaidia hata kupunguza rushwa na udanganyifu.
Prof. Kahyarara ametumia fursa hii kuwashukuru wabia wa maendeleo Trade Mark East Afrika (TMEA) ambao wamefadhili kuwaweka pamoja wataalamu wa kuandaa mfumo huu na sasa nchi yetu inaenda kunufaika kwani wawekezaji watazidi kuja kwa wingi kwani urasimu utapungua kwa kiasi kikubwa.
Naye mratibu wa mradi wa uaandaaji wa mfumo wa dirisha moja kwa wawekezaji (One Stop Centre) Bw. Robert John Mtendamema amesema kuwa kituo cha uwekezaji nchini kilianzishwa mwaka 1997 kikiwa na lengo la kuwahudumia wawekezaji kwa haraka chini ya mwamvuli wa dirisha moja (One stop shop) ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zinahudumia wawekezaji zimeweka maafisa ambao wana uwezo wa kutoa maamuzi ya kutoa vibali hivyo.
Bw. Mtendamema ameongeza kwa kusema kuwa kutokana na kukua kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya TEHAMA kila taasisi ndani ya One Stop Centre wameweza kuwa na mfumo wa kutoa kutoa huduma mbalimbali ambapo mwekezaji anapofika TIC inamuhitaji kuingia katika mifumo isiyopungua 12 ya kila taasisi yenye nywila tofauti kwa ajili ya kufanya maombi.
Bw. Mtendamema amesema kuwa kupitia mfumo huu unaoundwa sasa utawezesha kuondoa kero mbalimbali kwa wawekezaji hasa zile za kumlazimisha mwekezaji kuingia katika mifumo mbalimbali kutafuta vibali na sasa ataingia katika dirisha moja na kukuta taasisi zote na kufanya maombi kwa wakati mmoja, pia kupitia mfumo huu utawarahisishia wawekezaji kufanya maombi ya vibali na hii itapelekea kuongezeka kwa wawekezaji nchini kwa sababu ya urahisi wa kufanya maombi ya vibali mbalimbali.