MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akiongozana na Watalaamu wabobevu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), Taasisi ya Watafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Dodoma na Bonde la Wami-Ruvu,wakitafuta mwarobaini wa kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akimsikiliza mbobevu katika masuala ya misitu kutoka Ndaki ya Misitu Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Prof. Salim Malionde wakati wa ziara ya kutafuta mwarobaini wa kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) Dk Revocatus Mushumbusi wakati wa ziara ya kutafuta mwarobaini wa kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Maji Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,jinsi watakavyoshirikiana na wataalamu katika kutafuta mwarobaini wa kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akizungumza mara baada ya kukagua eneo la kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma ambapo aliongozana na Watalaamu wabobevu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), Taasisi ya Watafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Dodoma na Bonde la Wami-Ruvu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri,akiwataka viongozi wa bonde hilo kusimamia azma hiyo ya kukijanisha bonde wakati wa ziara ya kukagua eneo la kupanda miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Maji Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,akielezea jinsi walivyojipanga kusimamia na kuunganisha utalaamu kuhakikisha mpango wa kupanda miti katika bonde hilo unafanikiwa.
Mbobevu katika masuala ya misitu kutoka Ndaki ya Misitu Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Prof. Salim Malionde,akizungumzia jinsi watakavyotoa ushauri na utalaamu kwa kamati ya usimamizi wa mradi huo ili kuhakikisha miti itakayopandwa inastawi.
Mkuu wa Kikosi cha JKT Makurupora Luteni Kanali Festo Mbanga, akiahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kuhakikisha mifugo haingii katika eneo hilo na wapo tayari kutumia vijana hao kuchimba mashimo hayo mara watakaposhauriana na uongozi wa bonde.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akimsikiliza Mzee Shaban Nyamo ambaye pamoja na wanakijiji wengine wanadai fidia ya ardhi waliohamishwa katika eneo hilo.
Katibu wa CCM Kata ya Makutupora Bw.Mrisho Juma,akimuomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka kusimamia na kutatua kero ya zaidi Kaya takribani 600 zilizokuwa zikiishi eneo la chanzo Cha Maji Mzakwe katika Kata za,Mndemu,Gawaye,Mchemwa,Chihanga,Makutupora,pamoja na Mndemu wanaoomba wameiomba kuwalipwa fidia zao.
………………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,amewataka watu wa Bonde la Mto Wami-Ruvu kuwa wasimamizi kwa kuandaa mpango wa ubunifu kwa kuanza maandalizi ya upandaji wa miti katika eneo la ekari 309 kwenye umbali wa kilometa 2.5 katika msimu wa mwaka 2022/2023.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya kukagua na kujionea upandaji miti katika bonde la Mzakwe ambalo ni chanzo cha maji yanayosambazwa katika Jiji la Dodoma
Mtaka aliongozana na Watalaamu wabobevu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), Taasisi ya Watafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Dodoma na Bonde la Wami-Ruvu walifikia muafaka na kutafuta mwarobaini wa kunusuru miti aliyopandwa na kupanda mingine itakayostahimili ardhi ya bonde hilo.
Mtaka amesema kuwa anaitaka Mamlaka ya Bonde la Mto Wami-Ruvu kuwa msimamizi na kufanya maandalizi kwa kuandaa mpango wa ubunifu utakaonesha matokeo chanya ya upandaji huo, kabla ya kupanda miti katika eneo lenye ekari 309 lenye urefu wa kilometa 2.5 na upana meta 500.
“Mpango huo wa maandalizi unatakiwa kuonesha hatua za kuandaa eneo, uchimbaji wa mashimo na uandaaji miche na kinapofika kipindi cha masika, miti hiyo inapandwe ili kukijanisha bonde hili Nzakwe,”amesema Mtaka
RC Mtaka amesema kuwa lazima utafutwe mwarobaini kuhakikisha miti inayopandwa hapo inakua, inadumu na kustawi bila kuharibu chanzo muhimu cha maji.
Mtaka amesema kuwa pamoja na miti iliyopandwa na Rais Samia mwaka 2017 baadhi kunusurika ni kwa sababu ya vijana wa JKT Makurupora wanamwagilia na kuilinda, lakini mingine katika maeneo jirani ama imeungua na moto, imekauka na mingine imeliwa na mifugo.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka wawakilishi wa wanakijiji walioondolewa katika eneo hilo na viongozi wao wafike wakiwa na nyaraka zote za kudhibitisha malalamiko yao katika kikao kitakachofanyika ofisini kwake.
Amesema kikao hicho kitakachofanyika ofisini kwake Jumatatu saa 10.00 jioni, kitawashirikisha viongozi wa taasisi zilizosimamia shughuli ya kuwaondoa ambao nao amewataka waje na nyaraka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema kuwa muasisi wa upandaji miti katika eneo hilo ni Rais Samia na Makamu wa Rais Mpango anafuata nyayo za muasisi huyo, hivyo wao kama mkoa na wilaya wanatakiwa kuhakikisha bonde hilo linakijanishwa.
Shekimweri amewataka viongozi wa bonde hilo kusimamia azma hiyo ya kukijanisha bonde kufanya maandalizi ya kupanda miti ya aina mbalimbali inayostahimili na kugawa maeneo ya miti ya mapambo, matunda, dawa, utalii na kivuli katika eneo hilo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Maji Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy amesema, wapo tayari kusimamia na kuunganisha utalaamu kuhakikisha mpango wa kupanda miti katika bonde hilo unafanikiwa.
Mhandisi Mmassy amesema kuwa pia wapo katika maandalizi kuhakikisha wanaweka alama na kuchonga barabara kuzunguka eneo lenye ukubwa wa kilometa 460 za mujibu ambazo hakuna kazi zozote kufanyika katika eneo hilo na kuonesha eneo la kilometa 470 za kuishi lakini bila kilimo, na kutofugia mifugo.
Naye mbobevu katika masuala ya misitu kutoka Ndaki ya Misitu Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Prof. Salim Malionde amesema kuwa wao wapo tayari kutoa ushauri na utalaamu kwa kamati ya usimamizi wa mradi huo ili kuhakikisha miti itakayopandwa inastawi.
Prof. Malionde amesema kuwa watatumia utalaamu wao katika kutoa mawazo kwenye kamati na mpango utakaondaliwa na kufuatilia utekelezaji wake katika kuhakikisha miti itakayopangwa inakua na kustawi katika eneo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) Dk Revocatus Mushumbusi amesema kuwa watatoa ushauri na kutambua miti inayofaa kupandwa katika aina ya udongo uliopo hapo na kushiriki kikamilifu katika kutoa mchango wa kiushauri na kuhakikisha utunzaji wa miti.
Dk.Mushumbusi amesema miti jamii ya Acacia imekuwa katika eneo hilo kwa muda na hivyo wamekubaliana kuipanda miti hiyo kwenye eneo hilo.
Mkuu wa Kikosi cha JKT Makurupora Luteni Kanali Festo Mbanga amesema kuwa watatoa ushirikiano wa hali ya juu na kuhakikisha mifugo haingii katika eneo hilo na wapo tayari kutumia vijana hao kuchimba mashimo hayo mara watakaposhauriana na uongozi wa bonde.