Mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji Tanzania (TPCF), Joseph Parsambei akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha .(Happy Lazaro)
………………………………………….
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.
Mashirika ya wafugaji wa asili wanaotetea haki za wafugaji Tanzania wameomba kuwepo kwa meza huru ya mazungumzo kati ya wananchi na Serikali ili kupata suluhisho la mgogoro wa ardhi katika Tarafa ya Ngorongoro ,Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale.
Wakitoa tamko hilo Jijini Arusha , kuhusu mgogoro wa ardhi katika wilaya ya Ngorongoro ,Mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji Tanzania (TPCF),Joseph Parsambei amesema kuwa, wao kama mashirika wanayotetea wafugaji wamekutana na kujadili mgogoro huo ambapo wamekubaliana njia pekee ya kutatua ni kukaa meza ya pamoja na kuzungumza kati ya pande zote mbili na kumaliza mgogoro huo.
Parsambei amesema kuwa, Ngorongoro ni wilaya mojawapo inayopatikana katika mkoa wa Arusha,na ni moja ya wilaya yenye jamii ya wafugaji , ambapo wilaya hiyo ina Tarafa tatu ambayo ni Loliondo,Sale na Ngorongoro.
Amesema kuwa,eneo la Loliondo lina takriban kilometa za mraba 4000 na eneo la Ngorongoro likiwa na takriban kilometa za mraba 8000 ambapo wakazi wa wilaya hiyo ni wafugaji wa asili ya jamii ya wamaasai,watemi barbaiki na wahzabe.
“Ardhi ya eneo la Loliondo /Sale linatumika kwa ajili ya maisha yao ya kila siku yaani ufugaji na vijiji husika zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji vijiji 1978 na kuwepo hapo kihalali,ambapo eneo hilo limekuwa likitumika na matumizi mengine yakiwepo utalii wa picha na uwindaji,na limekuwa na mgogoro wa muda mrefu Kati ya watumiaji , ikiwepo ufugaji ,na uwindaji na utalii.”amesema.
Naye Msaidizi wa kisheria kutoka shirika linalotoa msaada wa kisheria la Equity Paralegal ( EPO ) Agness Marmo amesema kuwa , kwa pamoja kama.mashirika hayo wanaomba Serikali pamoja na wananchi wakae meza moja ya majadiliano na kuweza kulimaliza hilo jambo na kuondoa mkanganyiko mkubwa uliopo na wakubaliane namna ya matumizi ya eneo hilo.
“Matumizi endelevu ya Ardhi ni suluhisho la eneo hilo ,hivyo basi wadau wote wajikite katika mrengu huu ili maslahi yote yaweze kulindwa ,huku tukiomba hatua zote zitakazochukuliwa na Serikali jamii katika ngazi zote ziweze kushirikiana.”Agnes.
Afisa mipango kutoka shirika linalotetea maswala ya wafugaji (MPDO),Amani Sekino amesema kuwa,kwa pamoja wanalaani udhalilishaji unaofanywa na watu wenye nia mbaya ,wakiwepo wanasiasa na baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya wakazi wa eneo la Ngorongoro na Loliondo/sale.
Amani ameongeza kuwa,ni vizuri pande zote zikaa pamoja na kuzungumza huku zikijielekeza kujibu hoja na sio kushambuliana kwa maneno makali maana hazina tija yoyote kwao.
“Sisi asasi za kiraia tunaendelea kuwa macho na kufuatilia kwa ukaribu sakata hili ,na tunataka kila upande uheshimu sheria za nchi haki za binadamu na utawala wa sheria.”amesema Amani.